Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Erling Haaland kama asipoondoka England hakuna rangi hatutaiona

HAALAND Pict


WAZUNGU wana usemi wao. They don’t make like them anymore. Kwamba? Kuna watu hawatengenezwi tena. Ni usemi wa majivuno kuwasifu watu wa zamani waliofanya mambo makubwa. Mambo maalumu.


Kwamba kila siku watu bora au watu maalumu wanapotea. Alan Shearer aliondoka katika mpira mwaka 2006 wakati Erling Braut Haaland akiwa na miaka sita tu. Nadhani hata yeye mwenyewe Shearer hakujua kwamba kuna mchezaji mwenzake wa Ligi Kuu England alikuwa amemzaa mtoto ambaye angeweza kuwa tishio kwa rekodi zake.


Na kilichobakia kwa sasa ni labda Haaland ahame kwenye Ligi Kuu England ili kuokoa rekodi za Shearer. Haaland alizaliwa katika Jiji la Leeds baba yake akiwa staa wa zamani wa Leeds na Manchester City, Alf Inge Haaland.

Mapema wiki hii Haaland alifunga bao lake la 100 katika Ligi Kuu England. Amekuwa mchezaji wa kwanza kufunga mabao 100 Ligi Kuu England kwa haraka zaidi. Ametumia mechi 111 kufunga mabao 100. Kabla ya hapo rekodi ya kufikia mabao 100 kwa haraka zaidi ilikuwa imewekwa na Shearer. Alitumia mechi 124.

PAZ 01

Kivuli kingine ambacho kinamfukuza Shearer akiwa sebuleni pindi anapomfikiria Haaland ni ile rekodi kubwa anayoishika ya kuwa Mfungaji Bora wa muda wote wa Ligi Kuu England. Shearer alistaafu soka akiwa amefunga mabao 260 Ligi Kuu England.

Shearer aliondoka na rekodi yake akiwa na umri wa miaka 36 akiwa ametumia miaka zaidi ya 25 kuweka rekodi hiyo. Haaland ndio kwanza ana miaka 25. Kwa ufungaji wake huu ni wazi kwamba kama akifikisha umri wa miaka 36 akiwa katika Ligi Kuu England anaweza kuwa ameiacha mbali rekodi ya Shearer.

Namuona Haaland akiifikia rekodi ya Shearer ndani ya miaka mitano tu ijayo. Kitu ambacho kitamuokoa Shearer rekodi yake isivunjwe ni kama Haaland akikumbana na pesa za Waarabu wa Riyadh. Vinginevyo ataifikia hii rekodi akiwa na umri wa miaka 30 tu.

PAZ 02

Bahati mbaya kwa Shearer ni kwamba kuna wachezaji wazuri ambao siku hizi wanaamua kubaki katika klabu ambazo hazina historia kubwa katika soka lakini zina pesa. Zamani wachezaji wa aina ya Haaland walikuwa wanatamani zaidi kucheza Barcelona au Real Madrid. Siku hizi jambo hilo limepungua.

Mfano ni mchezaji kama Kevin de Bruyne. Zamani angeishia kucheza Real Madrid, lakini hadi uwezo wake unapungua uwanjani aliendelea kubaki Manchester City. Alipopungua zaidi hakuwa tena katika nafasi ya kucheza Real Madrid wala Barcelona akaenda zake Napoli.

PAZ 03

Manchester City kwa sasa wana uwezo wa kumpa Haaland pesa anayotaka, lakini pia akaendelea kukusanya vikombe. Uwezekano wa yeye kucheza hapo kwa muda mrefu upo na hii sio habari nzuri sana kwa Shearer.

Rekodi nyingine ambayo Haaland ameiweka rehani kwa wakubwa waliopita England ni ile inayoshikiliwa na Sergio Kun Aguero. Rekodi ya kufunga hat trick nyingi. Aguero hadi sasa anaongoza kwa kufunga hat trick nyingi katika Ligi Kuu England akiwa amefunga hat trick 12. Anafuatiwa na Shearer mwenye 11 huku Robbie Fowler akiwa nazo tisa.

Haaland amefikisha hat tricks nane akiwa anaungana na Thierry Henry, Harry Kane na Michael Owen. Wakati Kane akiwa anacheza Ujerumani, Henry na Owen wamestaafu soka. walio mbele ya Haaland pia wote wamestaafu soka.

PAZ 04

Kwa namna ambavyo anafunga kwa sasa nadhani hadi wakati Haaland anaivunja rekodi ya Shearer ni wazi kwamba atakuwa ameshaivunja rekodi ya Kun Aguero. Haaland anafunga mabao mengi ndani ya mechi moja. Ni tofauti na washambuliaji wengi wa kileo.

Hata hivyo, rekodi ya mabao ya Haaland inatuacha mdomo wazi kidogo na huwa inazua mjadala. Ni kweli kwamba anafunga mabao mengi kwa sababu mabeki wakali na wenye roho mbaya wameondoka katika Ligi Kuu England. Kwa sasa hatuna tena kina Nemanja Vidic, Sol Campbell, Rio Ferdinand, John Terry na wengineo. Hata katika klabu nyingine za kawaida kulikuwa na mabeki wenye roho mbaya. Ina maana Haaland angekuwa na wakati mgumu wa kufunga mabao kama angekuwa anacheza nyakati zile? Huu ni mjadala mwingine.

PAZ 05

Binafsi naamini bado Haaland angefunga tu. Haonekani kufunga mabao mengi kwa kuibia kama ilivyokuwa kwa kina Ruud Van Nistelrooy. Haaland anaonekana kuwa mchanganyiko kwa Thierry Henry kwa maana ya kasi, lakini anaonekana kuwa Van Nistelrooy kwa maana ya uwezo mkubwa wa jicho la lango, lakini papo hapo anaonekana kuwa kama Didier Drogba kwa matumizi ya nguvu.

Hata hivyo, upande mwingine una mawazo mengine. Mpira wa siku hizi umekuwa wa kimfumo zaidi katika ukabaji na mengineyo. Inawezekana pia washambuliaji wengi wa zamani wasingeweza kufunga mabao mengi katika mpira wa kisasa. Mbona Haaland anafunga?

Mwisho wa siku ni vyema tu tukiamua kuwa upande wake. Dunia inamshuhudia mmoja kati ya wafungaji hatari zaidi kuwahi kutokea katika uso wa ulimwengu. Naiona rekodi ya Shearer ikiteketea labda yeye na baba yake waamue kuona inatosha na waende kufuata pesa za Waarabu pale Riyadh.

Usemi wa kwamba ‘they don’t make like them anymore’ unapoteza maana unapoona Haaland akifunga kuliko Shearer alivyokuwa anafanya. Na hata yeye atakapoondoka itachukua muda kidogo kumpata kama yeye. Katika dunia hii inayopoteza washambuliaji kila kukicha nadhani Haaland ataacha pengo pindi akiondoka katika mpira.