Refa wa Inter Milan V Barca atoa majibu

Muktasari:
- Refa huyo wa fainali za Kombe la Dunia alishambuliwa na vyombo vya habari vya Barcelona kwamba alifanya matukio ya kuibana Barca, huku gazeti la Mundo Deportivo likifikia hatua mbaya ya kudai Marciniak ana urafiki wa kihistoria na Real Madrid.
WARSAW, POLAND: REFA wa Poland, Szymon Marciniak amejibu tuhuma za kwamba amewazuia Barcelona kutinga fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kuwabana kwenye baadhi ya matukio katika kipute cha nusu fainali dhidi ya Inter Milan.
Refa huyo wa fainali za Kombe la Dunia alishambuliwa na vyombo vya habari vya Barcelona kwamba alifanya matukio ya kuibana Barca, huku gazeti la Mundo Deportivo likifikia hatua mbaya ya kudai Marciniak ana urafiki wa kihistoria na Real Madrid.
Barca inalalamikia bao la kusawazisha la Inter lililofungwa na Francesco Acerbi na kulazimisha mechi hiyo kuingia kwenye dakika 30 za ziada, kwamba halikupaswa kukubalika kwa sababu beki wao wa pembeni Gerard Martin alifanyiwa rafu na Denzel Dumfries, aliyekwenda kupiga krosi ya bao hilo.
Miamba hiyo ya Hispania ilidai pia VAR haikupaswa kuipa penalti Inter kwa sababu Pau Cubarsi alipolala yombo aligusa mpira kwanza kabla ya Lautaro Martinez kujiangusha ndani ya boksi na kumpa nafasi Hakan Calhanoglu kufunga kwa mkwaju huo wa penalti. Na kwamba aliinyima penalti kadhaa Barca pale Yamal alipofanyiwa faulo na pia beki wa Inter aliposhika mpira ndani ya boksi.
Akizungumza kujibu tuhuma hizo za Barcelona, mwamuzi Marciniak aliambia Al Qahera: “Niseme nini juu ya hizi komenti za kijinga? Sijamkosea yeyote.”
Barca ilidai kwamba itafungua malalamiko rasmi Uefa, lakini mwamuzi Marciniak wala hatishiki na kujibu: “Nipo tayari kwa lolote.”
Marciniak alizungumzia pia bao la tatu la Inter, akisema: “Bao lile la tatu la Inter halikuwa na shida yoyote.”
Kocha wa Barcelona, Hansi Flick alisema baada ya mechi hiyo ya San Siro: “Sitaki kuzungumza sana kuhusu refa, lakini kila kitu alifanya kuwapendelea Inter. Nimehuzunika. Sipendi sana kumzungumzia refa. Nilishamwambia nilichokuwa nakifikiria, lakini siwezi kukisema.”
Kocha wa zamani wa Arsenal, Arsene Wenger akichambua mechi hiyo alisema penalti ya Martinez, haikuwa sahihi.
Wenger alisema: “Ni wazi kabisa Lautaro Martinez alikuwa akitafuta penalti kwa maoni yangu na refa alikosea kutoa penalti. Angetezama nani amegusa mpira kwanza, nani alifika kwenye tukio kwanza. Alikuwa Cubarsi. Kwangu mimi ile sio penalti.”