Liverpool yamtaka Kevin De Bruyne

Muktasari:
- Mbelgiji huyo atamaliza mkataba wake mwishoni mwa msimu huu akizifikisha mwisho zama zake kwenye kikosi cha Man City baada ya kudumu kwa miaka 10 katika chama hilo la Etihad.
MANCHESTER, ENGLAND: KIUNGO mchezeshaji wa Manchester City, Kevin De Bruyne amepata ofa ya kushtukiza ya kubaki kwenye Ligi Kuu England baada ya Liverpool kuhitaji huduma yake akakipige huko Anfield, imeelezwa.
Mbelgiji huyo atamaliza mkataba wake mwishoni mwa msimu huu akizifikisha mwisho zama zake kwenye kikosi cha Man City baada ya kudumu kwa miaka 10 katika chama hilo la Etihad.
De Bruyne anahitaji kubaki kwenye soka la Ulaya kuliko kwenda kukipiga Marekani au Saudi Arabia. Na klabu kadhaa kubwa zingependa kuwa na huduma ya mchezaji huyo kwenye timu yao.
Kwa mujibu wa Gianluca Di Marzio, alisema miongoni mwa timu zinazotaka De Bruyne ni Napoli.
Hata hivyo, kuna ofa pia ya kumbakiza kwenye Ligi Kuu England baada ya Liverpool kuhitaji saini yake. De Bruyne kwenye nyakati zake bora katika kikosi cha Man City alikuwa akichuana kuwania ubingwa dhidi ya Liverpool.
Kocha wa Liverpool, Arne Slot anataka kufanya maboresho makubwa kwenye safu ya kiungo ya timu yake na ndiyo maana anapiga hesabu za kwenda kunasa saini ya De Bruyne. Liverpool inajiandaa kutoa pesa kusajili wakali wapya kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi. Kiungo, De Bruyne ameripotiwa kuwa kwenye rada za Aston Villa pia.
Staa huyo alitua Etihad mwaka 2015, amecheza mechi 418 akifunga mabao 108 na asisti 177.