Refa wa Arsenal atumiwa meseji mbaya, zachunguzwa
Muktasari:
- Refa huyo alimtoa kwa kadi nyekundu staa wa Arsenal, Myles Lewis-Skelly katika mechi ambayo Gunners ilishinda 1-0 dhidi ya Wolves katika Ligi Kuu England wikiendi iliyopita.
LONDON, ENGLAND: POLISI imeanzisha uchunguzi baada ya mwamuzi wa soka Michael Oliver kutumiwa meseji za vitisho.
Refa huyo alimtoa kwa kadi nyekundu staa wa Arsenal, Myles Lewis-Skelly katika mechi ambayo Gunners ilishinda 1-0 dhidi ya Wolves katika Ligi Kuu England wikiendi iliyopita.
Uamuzi huo ulionekana kuwa wa utata, lakini VAR haikutumika kubatilisha kadi hiyo. Beki huyo mwenye umri wa miaka 18, alimkanyaga Matt Doherty alipokuwa anachomoka na mpira kuelekea kwenye goli la Arsenal.
Picha za marudio za picha mjongeo zilionyesha njumu za staa huyo wa Arsenal kumgusa mchezaji wa Wolves.
Ligi Kuu England ilithibitisha kwamba VAR iliunga mkono uamuzi wa mwamuzi kwa sababu Lewis-Skelly alionekana kucheza rafu mbaya.
Na sasa PGMOL imetoa taarifa kwamba polisi inaanza uchunguzi juu ya meseji za vitisho anazotumiwa mwamuzi huyo.
Taarifa hiyo ilisomeka hivi: “Tunasikitishwa na meseji za vitisho na matusi zinazoelekezwa kwa mwamuzi Michael Oliver baada ya mechi ya Wolverhampton Wanderers v Arsenal. Hakuna refa anayepaswa kukumbana na matusi, lakini ameshambuliwa yeye na familia yake ndani ya saa 24 zilizopita.
“Polisi inafahamu hilo na imeanza uchunguzi. Tunamsapoti Michael, sote tumeguswa na jambo hilo na tupo tayari kupambana na hizi tabia. Bahati mbaya hii si mara ya kwanza kwa waamuzi kukutana na meseji za vitisho. Tutaendelea kuunga mkono uchunguzi huu.”
Staa wa zamani wa Tottenham, Jamie Redknapp alipinga unyanyasaji kwa refa Oliver, aliposema: “Ni upuuzi mkubwa. Tumefikia hatua mwaka mwamuzi anapokuwa sahihi basi yupo sahihi, lakini anapofanya makosa basi amekula rushwa. Kama tutaendelea hivi basi hatutakuwa na waamuzi vijana watataka hii kazi. Michael Oliver ni mwamuzi bora sana. Kila mtu anafanya makosa.”