Real Madrid yavamia kwa Wharton
Muktasari:
- Kiungo huyo wa England, 21, amekuwa kwenye rada za klabu za Manchester United, Manchester City na Liverpool kwa muda mrefu sasa.
MADRID, HISPANIA: REAL Madrid imeingia kwenye mbio za kufukuzia saini ya staa wa Crystal Palace, Adam Wharton kwa mujibu wa taarifa kutoka Marekani.
Kiungo huyo wa England, 21, amekuwa kwenye rada za klabu za Manchester United, Manchester City na Liverpool kwa muda mrefu sasa.
Man United inapewa nafasi kubwa mbele ya vigogo hao wengine kwenye dirisha hili, huku ikiangalia chaguo rahisi zaidi baada ya Brighton kuhitaji Pauni 115 milioni kwenye mauzo ya kiungo mkabaji Carlos Baleba.
Hata hivyo, miamba ya LaLiga, Real Madrid sasa imeingia kwenye mchakato huo wa kuhitaji saini ya kiungo Wharton. Kocha wa Los Blancos, Xabi Alonso, anahitaji kiungo wa chini baada ya kumkosa Martin Zubimendi, aliyetimkia Arsenal. Madrid ina viungo wengi kama Jude Bellingham, Eduardo Camavinga, Fede Valverde, Aurelien Tchouameni na Dani Ceballos, lakini bado inasaka mrithi wa kudumu wa Luka Modric.
Na kwa Wharton, miamba hiyo ya Hispania inaamini itakuwa imepata mtu sahihi. Akiwa na umri wa miaka 21, kiungo huyo anayetumia mguu wa kushoto, amekuwa na uwezo mkubwa wa kumiliki kasi na ari ya mtoto.
Hata hivyo, tatizo linaloikabili Madrid ni kwamba huenda ikashindwa kuweka ofa yao rasmi mezani baada ya usajili wa Trent Alexander-Arnold, Dean Huijsen, Franco Mastantuono na Alvaro Carreras na kwamba Los Blancos kufanya usajili huo kabla ya dirisha kufungwa Septemba 1, italazimika kuuzwa kwanza.
Na mchezaji ambaye wanaweza kumuuza ni winga wa Kibrazili, Rodrygo, ambaye yupo kwenye rada za Liverpool, Man City, Arsenal na Tottenham, huku thamani yake ikidaiwa kuwa kati ya Pauni 70 milioni na Pauni 80 milioni.
Na kuhusu Wharton, klabu yake ya Palace haiwezi kukubali kupokea simu yoyote kwa ada isiyofika na kuzidi Pauni 69 milioni.