Real Madrid yatoa majibu kuhusu Endrick
Muktasari:
- Uongozi wa Real Madrid umeweka msimamo kuwa Endrick ambaye kwa sasa yupo kwa mkopo wa msimu mzima Olympique Lyon, atarejea Santiago Bernabeu mwishoni mwa msimu huu na kuunganishwa moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza msimu ujao.
ARSENAL, Chelsea na Tottenham Hotspur zimeambiwa aziwezi kumpata mshambuliaji chipukizi wa Brazil, Endrick, 19, katika dirisha lijalo la kiangazi.
Uongozi wa Real Madrid umeweka msimamo kuwa Endrick ambaye kwa sasa yupo kwa mkopo wa msimu mzima Olympique Lyon, atarejea Santiago Bernabeu mwishoni mwa msimu huu na kuunganishwa moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza msimu ujao.
Real Madrid inamuona Endrick kama sehemu muhimu ya mipango na imevutiwa na kiwango alichoonyesha tangu ajiunge na Lyon.
Tangu ajiunge na Lyon, Endrick amecheza mechi tisa za michuano yote akifunga mabao matano na asisti moja.
Mkataba wa sasa wa Endrick na Real Madrid unatarajiwa kumalizika 2030.
Awali, Madrid ilimruhusu mchezaji huyo atimkie Lyon ili akapate nafasi zaidi ya kucheza na sasa inaonekana mpango umeenda vizuri kwani ameanza kuonyesha kiwango bora ambacho alikionyesha akiwa na Palmeiras kabla hajatua Hispania.
Dayot Upamecano
BEKI wa kimataifa wa Ufaransa, Dayot Upamecano, 27, amevunja kabisa matumaini ya Liverpool na Real Madrid zinazotaka kumsajili baada ya kusaini mkataba mpya na Bayern Munich utakaomuweka katika kikosi hicho kwa muda mrefu zaidi. Upamecano alikuwa akihusishwa kuondoka katika viunga vya Allianz Arena tangu Januari, mwaka huu, ambapo Liverpool na Real Madrid ziliripotiwa kutaka kumsajili. Hata hivyo, uongozi wa Bayern umembakisha.
Igor Thiago
VIGOGO wa soka Ulaya, Manchester City, Chelsea na Bayern Munich bado wanaendelea kumfuatilia kwa karibu mshambuliaji wa kimataifa wa Brazil, Igor Thiago, 24, licha ya mchezaji huyo kusaini mkataba mpya na Brentford. Thiago amekuwa akionyesha kiwango cha juu tangu ajiunge na Brentford, jambo lililomfanya kuwa miongoni mwa washambuliaji waliowindwa sana tangu dirisha lililopita la majira ya kiangazi. Inaelezwa kuwa klabu hizo zinatuma maskauti.
Wesley Franca
MANCHESTER City ipo tayari kuwasilisha ofa ya takribani Euro 50 milioni 50 ili kumsajili beki wa kulia wa kimataifa wa Brazil, Wesley Franca, 22, kutoka AS Roma katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Wesley amekuwa akionyesha kiwango cha juu katika Serie A jambo lililovutia benchi la Man City linalotaka kusuka upya safu ya ulinzi ambayo imekuwa na changamoto ya majeraha ya mara kwa mara ambayo yanachangiwa na kutumika sana.
Marcus Rashford
BARCELONA imeomba kupunguziwa ada ya Pauni 26 milioni iliyokubaliwa awali ya kumsajili kwa mkataba wa moja kwa moja mshambuliaji wa Manchester United, Marcus Rashford, 28, ambaye kwa sasa anacheza kwa mkopo katika kikosi chao. Hata hivyo, Man United imeshikilia msimamo wa kutopunguza ada hiyo ya uhamisho na kuiambia Barca kuwa ikishindwa kutoa itamuuza sehemu nyingine. Kwa sasa Barcelona inajaribu kupata suluhisho.
Andre Onana
MANCHESTER United ipo tayari kumuuza kipa wa kimataifa wa Cameroon, Andre Onana, 29, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi ambaye kwa sasa anacheza kwa mkopo katika Trabzonspor ya Ligi Kuu Uturuki. Onana alipoteza nafasi chini ya kocha Ruben Amorim akakubali kwenda kwa mkopo Uturuki kwa ajili ya kupata muda mwingi wa kucheza. Uongozi wa Man United unaamini kumuachia kutaipunguzia mzigo.
Aleksandar Stankovic
INTER Milan imepanga kutumia kipengele cha kumnunua tena kiungo wake wa zamani Aleksandar Stankovic, 20, anayeichezea Brugge ya Ubelgiji, licha ya ushindani mkubwa kutoka kwa vigogo wa Ligi Kuu England. Stankovic, raia wa Serbia, aliuzwa Brugge majira ya kiangazi mwaka jana lakini Inter iliweka kipengele kinachoeleza kuwa inaweza kumnunua kwa Pauni 20 milioni.
Nico Paz
REAL Madrid imeamua kutumia kipengele cha kumnunua tena kiungo wa kimataifa wa Argentina Nico Paz, 21, kutoka Como ya Italia katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Paz ambaye alijiunga na Como akitokea Real Madrid amekuwa akifanya vizuri katika Serie A kiasi cha kuwavutia mabosi wa Bernabeu kutaka kumrudisha.Uongozi wa Madrid unamuona ni sehemu ya mkakati wa kuendelea kuimarisha kikosi.