Real Madrid yatishia kujitoa La Liga
Muktasari:
- Miamba hiyo kwa sasa inaongoza msimamo wa ligi hiyo na kujiweka kwenye nafasi ya kunyakua taji.
MADRID, HISPANIA: REAL Madrid imefikiria mpango wa kujitoa kwenye La Liga, imeelezwa.
Miamba hiyo kwa sasa inaongoza msimamo wa ligi hiyo na kujiweka kwenye nafasi ya kunyakua taji.
Lakini, miamba hiyo ya Bernabeu, imeripotiwa kuwa na tatizo na rais wa LaLiga, Javier Tebas na bodi ya waamuzi. Real Madrid inalalamika imekuwa haitendewi haki na waamuzi kwenye mechi zao.
Hiyo ikiwamo na pamoja na mchezaji wa timu pinzani Carlos Romero kutoonyeshwa kadi nyekundu baada ya kumchezea rafu Kylian Mbappe katika mechi ya kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Espanyol.
Romero alibaki uwanjani na kufunga bao la ushindi katika mechi hiyo.
Uongozi wa Real Madrid ulilalamikia jambo hilo, lakini Tebas aliwajibu kwa kuwaambia "wamerukwa na akili".
Kingine kuna malalamiko ya kuhusu kadi nyekundu aliyoonyeshwa Jude Bellingham katika mchezo wa wikiendi iliyopita dhidi ya Osasuna.
Kocha wa Carlo Ancelotti alipiga kijembe akisema "VAR lazima itakuwa ilizimwa" wakati kiungo huyo wa England akikabiliwa na adhabu ya kufungiwa mechi 12.
Real Madrid ilitoka sara 1-1 kwenye mechi hiyo na hivyo kuipa nafasi Barcelona ya kuwavuka endapo kama itashinda dhidi ya Rayo Vallecano kwenye mchezo wao wa usiku wa Jumtatu.
Waamuzi wa LaLiga walifichua watafanya mgomo endapo kama malalamiko ya Real Madrid dhidi yao yataungwa mkono na hayatachukuliwa hatua.
Katika ripoti nyingine imefichua Real Madrid sasa inafikiria kujitoa kutoka kwenye La Liga na kuhamia kwenye ligi ya nchi nyingine.
Katika kulifanya jambo hilo kutimia, rais wa klabu hiyo, Florentino Perez atahitaji uthibitisho kutoka Fifa.
Atalazimika kutuma maombi ya kuhama mashindano huku pia mchakato huo utahitaji baraka za La Liga.
Bellingham alionyeshwa kadi nyekundu baada ya kushindwa kuelewana lugha na mwamuzi wa mchezo wao dhidi ya Osasuna. Kiungo huyo alitoa matamshwi, ambayo kwa mwamuzi, ose Munuera aliyatafsiri ametukanwa.
Mwamuzi huyo aliandika jambo hilo kwenye ripoti yake kitu kinachomweka Bellingham kwenye hatari ya kufungiwa mechi 12, ambazo zitamfanya awe nje ya uwanja kwa sehemu kubwa ya mechi zilizobaki msimu huu.