Real Madrid yaruka kimanga kwa Olise
Muktasari:
- Klabu hiyo imesema haijawahi kuwa na mawasiliano yoyote ya moja kwa moja au yasiyo ya moja kwa moja na mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24, wala na wawakilishi wake au watu wa karibu naye, kufuatia ripoti zilizodai kuwa Real Madrid ilikuwa ikifikiria kutoa zaidi ya euro200 milioni kwa ajili ya usajili wake.
MADRID, Hispania: Real Madrid wamekanusha taarifa zilizokuwa zikiwahusisha na winga wa Bayern Munich na timu ya taifa ya Ufaransa, Michael Olise.
Klabu hiyo imesema haijawahi kuwa na mawasiliano yoyote ya moja kwa moja au yasiyo ya moja kwa moja na mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24, wala na wawakilishi wake au watu wa karibu naye, kufuatia ripoti zilizodai kuwa Real Madrid ilikuwa ikifikiria kutoa zaidi ya euro200 milioni kwa ajili ya usajili wake.
Katika taarifa yao rasmi, Real Madrid walisisitiza kuwa: “Real Madrid pia inapenda kusisitiza uhusiano bora wa kiutawala uliopo kati yake na Bayern Munich, na inasikitishwa na kuenea kwa taarifa za kubahatisha ambazo hazina ukweli.”
Klabu hiyo iliongeza kuwa iwapo kutakuwa na nia ya kumsajili mchezaji wa klabu nyingine, mazungumzo yanapaswa kwanza kufanyika kati ya klabu husika kabla ya hatua nyingine yoyote.
Olise alikuwa na msimu bora wa 2025/26, akifunga mabao 22 na kutoa pasi 31 za mabao katika mashindano yote akiwa na Bayern Munich. Pia ni sehemu muhimu ya kikosi cha Ufaransa katika Kombe la Dunia 2026.
Katika mechi yao ya kwanza ya hatua ya makundi dhidi ya Senegal, Olise alitoa pasi ya bao la kwanza lililofungwa na Kylian Mbappe katika ushindi wa mabao 3-1.
Wakati huo huo, Real Madrid chini ya kocha mpya Jose Mourinho tayari wamefanya usajili kadhaa muhimu msimu huu. Wamemsajili Bernardo Silva kwa uhamisho wa bure, Marc Cucurella kutoka Chelsea kwa pauni52 milioni, na pia wanatarajiwa kumpata Ibrahima Konate baada ya mkataba wake na Liverpool kumalizika mwishoni mwa mwezi huu.
Hata hivyo, Real walipata pigo baada ya ofa yao ya euro150 milioni kwa mshambuliaji Julian Alvarez kukataliwa na mahasimu wao wa jiji, Atlético Madrid.
Ofa hiyo ilikuja baada ya rais wa klabu, Florentino Perez, kuahidi wakati wa kampeni za uchaguzi kwamba angewasilisha ofa ya euro150 milioni kwa ajili ya kumsajili nyota mmoja mkubwa wa kiwango cha ‘Galactico’ ikiwa angechaguliwa tena.
Perez alishinda uchaguzi huo kwa kupata asilimia 65 ya kura na ataendelea kuwa rais wa Real Madrid hadi mwaka 2030.