Liverpool yakataa ofa ya Inter Milan
Muktasari:
- Ofa hiyo iko chini ya thamani ambayo Liverpool imeweka kwa mchezaji huyo, ambayo ni pauni35 milioni, na klabu hiyo haiko tayari kumuuza kwa bei ya chini.
LONDON, England: Liverpool imekataa ofa ya maneno yenye thamani ya euro25 milioni 25 kutoka Inter Milan kwa ajili ya kiungo Curtis Jones.
Ofa hiyo iko chini ya thamani ambayo Liverpool imeweka kwa mchezaji huyo, ambayo ni pauni35 milioni, na klabu hiyo haiko tayari kumuuza kwa bei ya chini.
Jones mwenye umri wa miaka 25 amebakiza mwaka mmoja tu katika mkataba wake wa sasa wa Anfield, na hii ni mara ya pili kwa Inter Milan kuonyesha nia ya kutaka kumsajili ndani ya mwaka huu.
Mwezi Januari, klabu hiyo ya Italia ilichunguza uwezekano wa kumpata Jones kwa mkopo wenye kipengele cha kumnunua baadaye, lakini pendekezo hilo pia lilikataliwa na Liverpool.
Mapema mwezi huu, mkurugenzi wa michezo wa Inter Milan, Piero Ausilio, alisema:”Curtis Jones tunamfuatilia kwa karibu. Hatukuficha hilo. Tunasubiri kuona maendeleo yatakavyokuwa.”
Aidha, nyota wa Inter Milan, Federico Chiesa, aliliambia gazeti la Italia La Gazzetta dello Sport kuwa Jones aliwahi kumuuliza maisha ya kuishi nchini Italia yakoje, jambo ambalo limeongeza uvumi kuhusu uwezekano wa kuhamia Serie A. Jones ni zao la akademi ya Liverpool. Alijiunga na mfumo wa vijana wa klabu hiyo akiwa na umri wa miaka tisa kabla ya kusaini mkataba wake wa kwanza wa kitaaluma mwaka 2018.
Kutokana na umuhimu wake katika kikosi na thamani ambayo Liverpool imeweka kwake, inaonekana Inter Milan italazimika kuongeza ofa yake kwa kiasi kikubwa ikiwa itataka kufanikisha usajili wa kiungo huyo wa England.