Real Madrid yaangukia kwa Enzo Fernandez

Muktasari:
- Enzo mwenye umri wa miaka 24, ili kuondoka Chelsea zitahitaji zaidi ya Euro 100 milioni kama ada yake ya uhamisho, kwani alisajiliwa kwa mkwanja mrefu alipotua Darajani majira ya kiangazi ya msimu wa 2023/24.
REAL Madrid imeanza mchakato wa kutaka kumsajili kiungo wa Chelsea na Argentina, Enzo Fernandez ambaye ameonyesha utayari wa kujiunga nayo katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi kwani ni moja kati ya ndoto za mchezaji huyo kukichezea kikosi hicho.
Enzo mwenye umri wa miaka 24, ili kuondoka Chelsea zitahitaji zaidi ya Euro 100 milioni kama ada yake ya uhamisho, kwani alisajiliwa kwa mkwanja mrefu alipotua Darajani majira ya kiangazi ya msimu wa 2023/24.
Mbali ya mwanja huo, kwa mujibu wa tovuti ya Four Four Two kuna uwezekano mkubwa yakafanyika mabadilishano ya wachezaji ambapo Aurelien Tchouameni anaweza kwenda Chelsea kisha Enzo kutimkia Real Madrid.
Mkataba wa sasa wa nyota huyo unatarajiwa kumalizika 2032. Katika msimu huu amecheza mechi 34 za michuano yote, akifunga mabao matano na kutoa asisti tisa.
Dean Huijsen
REAL Madrid inataka kumsajili beki wa kati wa Bournemouth na timu ya taifa ya Hispania, Dean Huijsen, 19, ambaye awali aliitumikia Uholanzi katika timu zake za vijana za taifa kabla ya kubadili upepo na kuitumikia Hispania. Mara kadhaa maskauti wa Real Madrid wamesafiri kwenda England kwa ajili ya kumtazama mchezaji huyo akiwa anaichezea Bournemouth katika Ligi Kuu England.
Morgan Gibbs-White
LIVERPOOL, Arsenal na Manchester United ni miongoni mwa timu zinazoitaka huduma ya kiungo wa Nottingham Forest na England, Morgan Gibbs-White, 25, ambaye zinaweza kumsajili katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi mwaka huu. Morgan amekuwa katika rada za vigogo kutokana na ubora aliouonyesha tangu msimu uliopita. Licha ya kuonyesha nia ya kumsajili Nottingham haionekani kuwa tayari kumuachia.
William Saliba
BEKI wa kati wa Arsenal, William Saliba hana mpango wa kuondoka katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi licha ya Real Madrid kuwa tayari kulipa ada ya uhamisho ya rekodi ya dunia ili kuipata huduma ya staa huyo wa kimataifa wa Ufaransa. Madrid ilianza kuhusishwa naye tangu dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana. Mkataba wake unamalizika 2027.
Tammy Abraham
STRAIKA wa AS Roma na England, Tammy Abraham, 27, ambaye anacheza kwa mkopo AC Milan anadaiwa kuwaambia watu wake wa karibu kuwa anataka kujiunga na Aston Villa dirisha lijalo la majira ya kiangazi na tayari mazungumzo ya wawakilishi wake na mabosi wa timu hiyo yameshaanza. Roma imemwambia hayupo katika mipango yao msimu ujao sawa na Milan ambayo haina mpango naye.
Angel Gomes
TOTTENHAM Hotspur ipo katika hatua nzuri kwenye mazungumzo na wawakilishi wa kiungo wa Lille, Angel Gomes juu ya kumsajili kama mchezaji huru katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi ambapo mkataba wake utakuwa unamalizika. Lille imeonyesha nia ya kutaka kumsainisha mkataba mpya lakini changamoto kubwa mwenyewe hataki kuendelea kubakia katika timu hiyo.
Nico Schlotterbeck
LIVERPOOL imeanza mazungumzo kwa ajili ya kumsajili beki wa Borussia Dortmund na Ujerumani, Nico Schlotterbeck, 25, ambaye anaonekana kama mbadala wa muda mrefu kwa Virgil van Dijk. Mabosi wa Liverpool wameanza kujiandaa na maisha bila Van Dijk kwa sababu mkataba unamalizika mwisho wa msimu na hadi sasa hawajakubaliana dili jipya.
Andy Robertson
LLIVERPOOL ipo mawindoni kutafuta beki atakayeziba pengo la Andy Robertson, 31, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi na mmoja kati ya iliowaweka katika rada ni staa wa kimataifa wa Hungary anayeichezea Bournemouth, Milos Kerkez, 21. Kerkez amekuwa katika rada za Liverpool kutokana na kiwango bora anachoonyesha.