Real Madrid mpya ya Mourinho usipime
Muktasari:
- Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari vya Hispania, Mourinho anaonekana kuwa karibu kurejea kuinoa Real Madrid baada ya miaka 13, hatua ambayo inaweza kuleta mapinduzi ndani ya kikosi hicho.
MADRID, HISPANIA: MIAMBA ya soka la Hispania, Real Madrid inaripotiwa kuingia kwenye kipindi kipya cha mabadiliko makubwa endapo Jose Mourinho atarejea Santiago Bernabeu huku mipango ya kikosi kipya ikijumuisha mabadiliko makubwa katika safu ya kiungo na ushambuliaji.
Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari vya Hispania, Mourinho anaonekana kuwa karibu kurejea kuinoa Real Madrid baada ya miaka 13, hatua ambayo inaweza kuleta mapinduzi ndani ya kikosi hicho.
Mabadiliko hayo yanaelezwa yanaweza kuanzia eneo la kiungo ambapo kiungo wa Manchester City, Rodri anatajwa kuwa chaguo la kwanza la Mourinho kama mhimili wa timu mpya.
Rodri ambaye bado ana nafasi ya kuondoka Manchester City iwapo atashindwa kuongeza mkataba wake, anaonekana kuwa mchezaji muhimu katika mpango wa kujenga upya Real Madrid, akitajwa kama mrithi wa majukumu ya kiungo wa ulinzi kama Casemiro alivyokuwa.
Katika mpango huo mpya, kiungo wa Chelsea, Enzo Fernández pia anatajwa kama mchezaji anayevutiwa na klabu hiyo ya Hispania, na angeunda kiungo kitakachokamilika pamoja na Rodri na Federico Valverde.
Mourinho anadaiwa kutaka kikosi chenye nguvu, nidhamu na kasi, ambapo Rodri angekuwa akicheza nafasi ya kiungo wa chini, Fernandez akiwa na jukumu la kupandisha mashambulizi huku Valverde akileta nguvu na kasi upande wa kulia wa kiungo.
Lakini mabadiliko makubwa zaidi yanaweza kuonekana kwenye safu ya ushambuliaji na nyota wa Real Madrid, Kylian Mbappe anatajwa huenda akawa na wakati mgumu katika mfumo mpya wa Mourinho.
Katika mpango huo, Vinicius Junior anaweza kubaki upande wa kushoto kama ilivyo kawaida huku Jude Bellingham akisogezwa juu zaidi kama kiungo mshambuliaji.