Real Madrid kumgeukia Enzo Fernandez kisa Rodri
Muktasari:
- Real Madrid inaonekana kuwa na mpango wa kuongeza nguvu katika eneo la kiungo msimu ujao ambapo inaamini linahitaji maboresho makubwa.
REAL Madrid inapanga kuhamia kwa kiungo wa Chelsea, Enzo Fernandez ikiwa itafeli kuipata saini ya staa wa Manchester City, Rodri, 29, katika dirisha lijalo la kiangazi.
Mbali ya Enzo, Madrid pia imemuweka katika rada zake kiungo wa Crystal Palace, Adam Wharton, 22, ambaye itaanza naye mazungumzo ya kumsajili ikiwa itamkosa Enzo.
Real Madrid inaonekana kuwa na mpango wa kuongeza nguvu katika eneo la kiungo msimu ujao ambapo inaamini linahitaji maboresho makubwa.
Kwa mujibu wa tovuti ya Football Insider inaweza kuigharimu Pauni 50 milioni ili kufanikisha mchakato wa kumsajili Rodri.
Mkataba wa sasa wa Rodri unatarajiwa kumalizika 2027. Miaka ya karibuni amekuwa akisumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara hali inayosababisha asipate muda mwingi wa kucheza.
Kwa upande wa Enzo, Chelsea inaonekana huenda ikawa tayari kumuuza.
Tino Livramento
MAZUNGUMZO ya mkataba mpya kati ya Newcastle United na beki raia wa England, Tino Livramento, 23, yanadaiwa kuwa yamekwama kutokana na kuhitaji mshahara mkubwa tofauti na ule ambao amewekewa mezani. Hali hiyo imefungua uwezekano wa mchezaji huyo kuondoka katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi ambapo timu nyingi zinaimezea mate huduma ya mchezaji huyo.
Julian Alvarez
BARCELONA ni miongoni mwa timu zinazodaiwa kuwa katika mazungumzo na wawakilishi wa mshambuliaji wa Atletico Madrid na Argentina, Julian Alvarez, 26, ambaye inataka kumsajili katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Barcelona inaonekana kuwa na nia ya kuimarisha safu ya ushambuliaji na Alvarez anaonekana kuwa chaguo bora kutokana na uwezo wake wa kufunga na uzoefu wake wa katika Ligi Kuu Hispania (La Liga).
Maxence Lacroix
LIVERPOOL itakutana na ushindani kutoka Bayern Munich katika mbio za kumsajili beki wa kimataifa wa Ufaransa, Maxence Lacroix, 25, anayekipiga Crystal Palace. Inaelezwa Bayern ipo tayari kutoa ofa nono zaidi ya ile ambayo Liverpool ilikuwa inajipanga kutoa hivyo kufanya mvutano uongezeke. Mkataba wa sasa wa Lacroix unatarajiwa kumalizika 2029. Msimu huu amecheza mechi 43 za michuano yote.
Lorenzo Lucca
BOLOGNA inapanga kufanya jaribio la kumsajili mshambuliaji wa Napoli, Lorenzo Lucca, 25, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Lucca kwa sasa yupo kwa mkopo wa msimu mmoja Nottingham Forest akitokea Napoli, na haonekani kuwa na mpango wa kusalia katika kikosi hicho. Bologna inaamini staa huyo ambaye msimu huu amefunga mabao matatu katika mechi 30 za michuano yote, atasaidia safu ya ushambuliaji.
Nathan Ake
BEKI wa Manchester City na timu ya taifa ya Uholanzi, Nathan Ake, 31, anatajwa kuwa anaweza kurejea katika klabu yake ya zamani, Chelsea kwenye dirisha lijalo. Inaelezwa Ake anafikiria kurejea Stamford Bridge ikiwa ni katika kutafuta changamoto mpya baada ya kudumu muda mrefu Man City. Mkataba wa sasa wa staa huyo unatarajiwa kumalizika mwakani. Tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi 27 za michuano yote.
Sandro Tonali
NEWCASTLE United imepata nafuu katika jitihada za kumbakisha kiungo Sandro Tonali, 25, kwa muda mrefu zaidi baada ya klabu nyingi za Serie A kuonyesha kujiondoa katika mchakato wa kutaka kumsajili baada ya kushindwa kumudu ada ya uhamisho. Hata hivyo, timu za Ligi Kuu England ambazo ni Man United na Man City zinamtamani Tonali kwa ajili ya kuboresha safu ya kiungo mwisho wa msimu kwani zinaweza kuondokewa na mastaa.
Manuel Ugarte
JUVENTUS inaendelea kumfuatilia kwa karibu kiungo wa kimataifa wa Uruguay, Manuel Ugarte, 24, anayekipiga Manchester United.
Inaelezwa kwamba Juventus imetuma maskauti mara kadhaa ili kumtazama Ugarte katika kipindi hiki cha mapumziko ya kimataifa, na ikiwa kila kitu kitakwenda sawa inaweza kuwasilisha ofa rasmi katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.Mchezaji huyo amekuwa hapati nafasi ya kutosha katika kikosi cha kwanza cha Man United.