Real Madrid, Bayern Munich zamvizia Dalot

Muktasari:
- Dalot ambaye ni mmoja kati ya mastaa wanaopata nafasi kubwa ya kucheza katika kikosi cha kwanza cha Man United chini ya Ruben Amorim, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2028.
BAYERN Munich na Real Madrid zimeonyesha nia ya kutaka kumsajili beki wa Manchester United na Ureno, Diogo Dalot, 25, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Dalot ambaye ni mmoja kati ya mastaa wanaopata nafasi kubwa ya kucheza katika kikosi cha kwanza cha Man United chini ya Ruben Amorim, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2028.
Inaelezwa kocha wa Bayern, Vincent Kompany ni mmoja kati ya mashabiki wakubwa wa beki huyu na anataka kumsajili kama mbadala wa Alphonso Davies ambaye mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu huu.
Kwa upande wa Madrid inamwangalia Dalot kama mpango wao wa pili ikiwa itashindwa kuinasa saini ya Trent Alexander Arnold, ambaye anamaliza mkataba wake na Liverpool mwisho wa msimu huu.
Nico Schlotterbeck
LIVERPOOL inafikiria kumsajili beki wa Borussia Dortmund na Ujerumani, Nico Schlotterbeck, mwenye umri wa miaka 25, ambaye anaonekana kama mbadala wa muda mrefu kwa Virgil van Dijk.
Mabosi wa Liverpool wameanza kujiandaa na maisha bila ya Van Dijk kwa sababu mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu na hadi sasa hawajafikia mwafaka juu ya kumuongeza mkataba mpya.
Viktor Gyokeres
LIVERPOOL, Manchester City na Arsenal ni miongoni mwa timu ambazo zinapewa nafasi kubwa ya kumsajili mshambuliaji wa Sporting Lisbon na Sweden, Viktor Gyokeres katika dirisha lijalo ikiwa staa huyo ataamua kuondoka mwisho wa msimu huu.
Gyokeres mwenye umri wa miaka 26, tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi 40 za michuano yote na kufunga mabao 39.
Dusan Vlahovic
MANCHESTER United huenda wakafanya usajili wa mshambuliaji Dusan Vlahovic baada ya Juventus kuwa tayari kupunguza bei yao ya Pauni 35 milioni waliyoiweka hapo awali.
Vlahovic ambaye mkataba wake unamalizika mwaka 2026, anahusishwa na Man United ambayo inatafuta mshambuliaji katika ikiwa ni kati maeneo ambayo yana upungufu tangu kuanza kwa msimu huu.
Angel Gomes
TOTTENHAM imeanza mazungumzo na wawakilishi wa kiungo wa Lille, Angel Gomes kuhusu mpango wa kumsajili staa huyu kama mchezaji huru katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi ambapo mkataba wake utakuwa unamalizika.
Lille imeonyesha nia ya kutaka kumsainisha mkataba mpya lakini changamoto kubwa ni kwa Gomes mwenyewe ambaye hahitaji kuendelea kubakia kwenye timu hiyo.
Kalvin Phillips
LEEDS imeshafanya makubaliano ya mdomo na wawakilishi wa Manchester City juu ya kumsajili kiungo wa timu hiyo na England, Kalvin Phillips ikiwa watafanikiwa kupanda Ligi Kuu England kwa msimu ujao.
Phillips mwenye umri wa miaka 29, kwa sasa anacheza kwa mkopo Ipswich Town, mkataba wake na Man City unatarajiwa kumalizika mwaka 2028.
Liam Delap
NEWCASTLE inataka kumsajili mshambualiji wa Ipswich Town, Liam Delap, mwenye umri wa miaka 22, ambaye ameendelea kuonyesha kiwango bora licha ya timu yake kutofanya vizuri msimu huu.
Delap ambaye amezivutia timu nyingi kubwa, msimu huu amecheza mechi 30 za michuano yote na kufunga mabao 10.
Arda Guler
OFA za AC Milan na Inter Milan zinadaiwa kumchanganya kiungo wa Real Madrid, Arda Guler ambaye anataka kuondoka ili kupata muda mwingi wa kucheza. Kijana wa Kituruki Arda Guler anataka kuondoka Real Madrid kwani anaendelea kushindwa kupata nafasi ya kucheza, huku Inter Milan na AC Milan wakiripotiwa kuvutiwa na kiungo huyo mwenye umri wa miaka 20.