Ratiba yaanza kuwa chungu Manchester City
Muktasari:
- Katika raundi ya nne, Arsenal na Man City zilipangiwa mechi zilizoonekana kuwa nafuu. Man City, japokuwa bila kushawishi sana, iliiondoa Salford City kwenye Uwanja wa Etihad, huku mabao manne ya kipindi cha kwanza yakiisaidia Arsenal kuichapa Wigan Athletic mabao 4-0.
MANCHESTER, ENGLAND: MATUMAINI ya Arsenal kutwaa taji la Kombe la Ligi yameongezeka baada ya Manchester City kufahamu wapinzani wao katika hatua ya tano ya Kombe la FA jambo linalowafanya kukabiliwa na ratiba ngumu kabia ya kukipiga kwenye fainali hiyo ya Carabao Cup.
Katika raundi ya nne, Arsenal na Man City zilipangiwa mechi zilizoonekana kuwa nafuu. Man City, japokuwa bila kushawishi sana, iliiondoa Salford City kwenye Uwanja wa Etihad, huku mabao manne ya kipindi cha kwanza yakiisaidia Arsenal kuichapa Wigan Athletic mabao 4-0.
Bahati iliendelea kwa upande wa Arsenal ilipopangiwa mechi ya ugenini dhidi ya Mansfield Town ya League One, ambao hivi karibuni waliiondoa Burnley. Lakini, kwa Man City ilipata droo ngumu wakipangwa kusafiri kucheza dhidi ya Newcastle United.
Tofauti na Arteta ambaye anaweza kuwapumzisha nyota wake na kutumia kikosi cha pili dhidi ya Mansfield, Guardiola atalazimika kuwatumia wachezaji wake wengi tegemeo kama ana nia ya kweli ya kutwaa taji la Kombe la FA.
Changamoto kwa Man City ni kwamba mechi hiyo itachezwa mwishoni mwa wiki ya Machi 7/8, wiki mbili kabla ya fainali ya Kombe la Ligi, huku tarehe kamili na muda wa kuanza mechi bado haujathibitishwa. Kabla ya hapo, Man City itakuwa na mechi ya nyumbani dhidi ya Nottingham Forest wanaopambana kutoshuka daraja, Machi 4. Pia itakuwa na safari ngumu ya ugenini dhidi ya West Ham United, Machi 14.
Kati ya safari ya Newcastle na West Ham, kutakuwa na michezo ya mkondo wa kwanza ya hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, Machi 10 na 11i. Man City itacheza dhidi ya mmoja kati ya Real Madrid, Benfica, Bodo/Glimt au Inter Milan, huku Arsenal ikipangwa kucheza dhidi ya Atalanta, Borussia Dortmund, Bayer Leverkusen au Olympiacos.
Man City ikijaribu kuikimbiza Arsenal, ambao hawajashinda taji kubwa tangu walipotwaa Kombe la FA 2020, ushindi dhidi ya wapinzani wao hao wa London Kaskazini katika fainali ya Kombe la Ligi utakuwa pigo kubwa kisaikolojia kwa kikosi cha Mikel Arteta.
Hata hivyo, mechi ya Kombe la FA dhidi ya Newcastle ni hatari. Kikosi cha pili cha Man City kinaweza kuwa katika hatari dhidi ya Magpies iwapo kocha Eddie Howe atawatumia nyota wake wote bora katika mashindano hayo, hivyo Pep Guardiola atalazimika kutumia mastaa wake wengi wa kikosi cha kwanza kabla ya kwenda kuwakabili Arsenal katika fainali ya Kombe la Ligi.