Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sapraizi 10 zinazoweza kutokea Ligi Kuu England 2025/26

MAAJABU Pict

Muktasari:

  • Na vitu vya kushtua vinavyotabiriwa ni kwamba huenda Mikel Arteta, Igor Tudor na Vitor Pereira wanaweza kumaliza vibaya msimu huu kwenye mikikimikiki hiyo ya Ligi Kuu England.

LONDON, ENGLAND: LIGI Kuu England imezidi kunoga huku kukiwa na sapraizi kibao zinazosubiriwa kabla ya mikikimikiki hiyo kufika ukingoni Mei mwaka huu.

Na vitu vya kushtua vinavyotabiriwa ni kwamba huenda Mikel Arteta, Igor Tudor na Vitor Pereira wanaweza kumaliza vibaya msimu huu kwenye mikikimikiki hiyo ya Ligi Kuu England.

Kinachoelezwa ni kwamba ubora wa Ligi Kuu England msimu wa 2025/26 umeshuka kiasi, lakini burudani na matukio makubwa hayajakosekana, huku ushindani ukiwa mkubwa zaidi kuliko mwaka uliopita.

Tofauti na misimu iliyopita, karibu kila kitu bado kinashindaniwa hadi katika hatua za mwisho; Wolves na Burnley zinaonekana kushuka daraja, lakini West Ham United imefufua vita ya kushuka daraja; Manchester City iko karibu na kileleni kuliko ambavyo vinara Arsenal wangependa; na ni vigumu kutabiri nani atafuzu kwa mashindano matatu ya Ulaya.

Hivyo basi, haya ni mambo kumi ya kushtua yanayoweza kutokea katika mechi 12 zilizobaki za msimu wa 2025/26 wa Ligi Kuu England.


MAAJ 01

1. Arsenal kukosa ubingwa wa Ligi Kuu

Kwa sasa, hakuna shaka kuwa kikosi cha kocha Mikel Arteta ndicho bora zaidi England na labda hata Ulaya, huku kikiwa na mkakati wa kumaliza ukame wake wa mataji kwa kutwaa angalau makombe mawili msimu huu kati ya manne inayoshindania hadi sasa.

Ubingwa wa Ligi Kuu England unaonekana kuwa sehemu ya mafanikio yao ya 2025/26, lakini haitakuwa rahisi kama ilivyoonekana miezi michache iliyopita.

Kumekuwa na mabadiliko ya kasi hivi karibuni, hasa baada ya ushindi mkubwa wa Man City ugenini dhidi ya Liverpool na sare ya Arsenal dhidi ya Brentford kuonyesha hali tofauti za timu hizo.

Sasa tofauti ni pointi nne tu kati ya Arsenal na Man City, pengo ambalo linatosha kukipa matumaini kikosi cha kocha Pep Guardiola kuwa historia inaweza kujirudia. Hilo likitokea ina maana Arsenal itakuwa imepoteza nafasi ya kuwa bingwa.


MAAJ 02

2. Man City washinde ubingwa

Arsenal imekuwa thabiti zaidi msimu huu na iko kileleni kwa sababu, lakini kinachovutia ni kuwa mbio za ubingwa hazijakuwa kamilifu; kosa moja tu litamaliza ndoto za Arsenal au Man City.

Kutakuwa na maswali mengi kwa Arteta kama ataanguka tena, hasa baada ya kutumia Pauni 250 milioni kwenye dirisha la kiangazi na kuwa na wachezaji bora katika kila nafasi.

Inawezekana presha ikawashinda Arsenal katika hatua za mwisho, lakini Man City nao sio wakamilifu. Kikosi hiki cha sasa cha Guardiola kinaweza kuwa dhaifu zaidi kuwahi kushinda taji ikiwa watafanikiwa.

Hata hivyo, uwepo wa wachezaji wa kiwango cha juu kama Erling Haaland na Gianluigi Donnarumma ni silaha muhimu. Usajili wa Januari wa Marc Guehi na Antoine Semenyo pia umeongeza nguvu, lakini bado timu hii ina upungufu. Itakuwa mafanikio makubwa kama itaipiku Arsenal katika kile kinachoweza kuwa msimu wa mwisho wa Guardiola.


MAAJ 03

3. Man United wamalize nafasi ya tatu

Uteuzi wa kuwa kocha wa mpito wa Manchester United, Michael Carrick umeenda vizuri zaidi ya matarajio ya mashabiki wa miamba hiyo ya Old Trafford, kiasi kwamba uongozi wa INEOS unaweza kujikuta kwenye wakati mgumu katika kipindi cha majira ya kiangazi kijacho iwapo atawaongoza kufuzu michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Tofauti na waliomtangulia, Carrick hakurithi timu iliyo katika vurugu; Ruben Amorim na wengine walifanya kazi ya kuweka msingi. Man United imefaidika na mabadiliko ya moja kwa moja aliyofanya Carrick na anastahili pongezi kwa kuiunganisha timu haraka.

Kwa kiwango kizuri cha Bruno Fernandes, Kobbie Mainoo na wenzake, pamoja na kutokuwa na mashindano ya kombe ya kuwasumbua, kumaliza nafasi ya tatu sasa inaonekana ni kitu kinachowezekana, huku jambo hilo lingeonekana kuwa gumu sana katika kipindi cha Amorim.


MAAJ 04

4. Aston Villa wakose tiketi ya Ligi ya Mabingwa

Aston Villa inaweza kukosa kabisa kufuzu mikikimikiki ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao na Manchester United inaweza kuchangia hilo kama ilivyofanya msimu uliopita.

Baada ya kelele za mapema za kumtaka kocha afutwe kazi, Unai Emery alifanya kazi ya ajabu katikati ya msimu huu huku Aston Villa ikionekana kutishia kuwania hata ubingwa wa Ligi Kuu England.

Hali hiyo ilifanya nafasi ya kufuzu Ligi ya Mabingwa ionekane kuwa ya uhakika. Hata hivyo, kushuka kwa kiwango katika mechi za karibuni kumezipa timu zilizo chini yao matumaini kuwa nafasi nyingine ya Ulaya inaweza kupatikana.

Kwa jinsi Liverpool inavyocheza, Aston Villa inapaswa kuwa salama angalau katika nafasi ya tano kutokana na pengo lao la pointi kuwa nane dhidi ya mabingwa hao watetezi. Lakini, hilo si la uhakika tena, hasa kutokana na majeraha yaliyoikumba vibaya safu ya kiungo ya wababe hao wa Villa Park.


MAAJ 05

5. Sunderland kufuzu mashindano ya Ulaya

Kwa kuzingatia mfumo wa kufuzu michuano ya Ulaya kwa klabu za Ligi Kuu England, Sunderland ina nafasi halisi ya kupata tiketi, iwe kwa kumaliza nafasi ya saba au kwa kushinda Kombe la FA.

Huenda “The Black Cats” ikaishia katikati ya msimamo, lakini ukweli kwamba mashabiki wao wanaweza hata kuota kucheza Ulaya unaonyesha walivyofanya vizuri msimu huu.

Timu iliyokuwa ikipewa nafasi kubwa ya kushuka daraja kabla ya msimu kuanza imekuwa ya kushangaza chini ya kocha, Regis Le Bris, kutokana na mbinu zake makini na usajili bora ulioandaa mwisho wa msimu wenye kusisimua.


MAAJ 06

6. Brentford kufuzu michuano ya Ulaya

Sunderland na timu nyingine zinaweza kupitwa katika mbio za kufuzu michuano ya UEFA Europa/ Conference League na Brentford, ambao kwa sasa wanaongoza mbio za kumaliza nafasi ya saba wakiwa na tofauti ya pointi tatu dhidi ya wanaowafuata kwa karibu.

Brentford, iliyokuwa ikipewa nafasi ya kushuka daraja kabla ya msimu kuanza, ilitabiriwa na wengi kuwa ingeshuka kiwango baada ya kuondoka kwa Thomas Frank pamoja na nyota kadhaa.

Hata hivyo, klabu hiyo inayotajwa kama inayoendeshwa vizuri zaidi nchini England, imefanikiwa licha ya changamoto hizo.

Keith Andrews ameonyesha kuwa yeye si kocha wa mipira ya adhabu tu, bali ameipeleka Brentford katika kiwango kingine akiwa na kikosi ambacho kwa wengi kinaonekana kuwa dhaifu zaidi kuliko kile kilichokuwa chini ya Frank msimu uliopita.


MAAJ 07

7. Brighton wamfukuze Fabian Hurzeler

Brighton pia imetajwa kama moja ya klabu zinazoendeshwa vizuri zaidi katika Ligi Kuu England, lakini mfumo wao umeanza kuonekana kuwa na upungufu kufuatia kushuka kwa kiwango msimu huu.

Licha ya kumuunga mkono kocha Fabian Hurzeler kwa matumizi ya Pauni 300 milioni, zaidi ya kocha yeyote aliyewahi kupewa, Brighton imerudi nyuma na kwa sasa inaanza kuangalia mabega yake baada ya kujikuta ikitajwa katika mjadala wa kushuka daraja.

Sasa kuna minong’ono kuwa Hurzeler yuko kwenye presha na amepewa nafasi kubwa ya kuwa kocha ajaye kufutwa kazi katika Ligi Kuu England. Vipigo viwili mfululizo dhidi ya Liverpool na Brentford vinaweza kuamua hatima yake, hasa ikizingatiwa kuwa ilikuwa ikionekana kuwania tiketi ya Ligi ya Mabaingwa Ulaya kwa kiwango cha Novemba mwaka jana.


MAAJ 08

8. West Ham United waepuke kushuka daraja

West Ham United ilionekana kama tayari imeshuka daraja kwa sehemu kubwa ya msimu huu, lakini sasa inaonekana kuwa timu kamili chini ya Nuno Espirito Santo, ambaye huenda akajivunia iwapo itaokoka huku Nottingham Forest wakishuka.

Nuno alionekana kama mtu aliyekata tamaa mwanzoni mwa mwaka alipokuwa karibu kufutwa kazi, lakini West Ham imefaidika kwa kumuunga mkono kocha huyo anayejulikana kwa kuokoa timu kwenye hatari. Usajili wao wa Januari umechangia pakubwa kuimarika kwao.

“The Hammers” ina ushindi mara tatu katika mechi tano zilizopita, na ingeweza kupata pointi zote kama si makosa ya dakika za mwisho dhidi ya Chelsea na Man United. Ingawa ina pengo la kuziba la pointi, inaonekana kuwa bora zaidi kati yao, Forest na Spurs na inaweza kufanya “muujiza wa kuokoka”.


MAAJ 09

9. Nottingham Forest wamfukuze Vitor Pereira

Vitor Pereira ni kocha wa nne wa kudumu wa Forest katika msimu wa 2025/26, akiwa amepewa mkataba hadi mwisho wa msimu ili kurudia kazi yake ya awali ya kuokoa timu kama alivyofanya Wolves.

Kuwa na makocha wanne wa kudumu katika msimu mmoja tayari ni rekodi ya Ligi Kuu England, lakini si ajabu kuona mmiliki tata Evangelos Marinakis akibonyeza tena kitufe cha taharuki kama uteuzi huu hautaleta matokeo ya haraka.

Kwa uhalisia, ni Marinakis mwenyewe anayehitaji kuwekwa mbali na Uwanja wa City Ground.


MAAJ 10

10. Tottenham Hotspur ishuke daraja

Kwa tofauti ya pointi 5 tu kati ya Tottenham na timu tatu za mkiani huku mechi 12 zikiwa zimesalia, klabu hiyo ya Kaskazini mwa London iko kwenye vita halisi ya kushuka daraja.

Spurs imechukua uamuzi wa hatari kwa kumteua Igor Tudor ili kuwaokoa, lakini kazi yake ya hivi karibuni huko Juventus inaashiria kuwa mambo yanaweza kwenda vibaya.

Mwisho wa yote, Spurs huenda ikawa na ubora wa kutosha katika kikosi chao kuipiku Forest na kuokoka. Hata hivyo, mechi ya Machi 22 kati ya timu hizi inaweza kuwa na athari kubwa sana katika mustakabali wa msimu wao.