Rasmi dilisha la usajili limefunguliwa, kazi inaanza!

Muktasari:
Klabu zilikuwa zikisubiri hesabu za kifedha za mwaka uliopita zifungwe, ambapo ilikuwa Jumatatu ya Juni 30 na sasa dili zote zitakazofanyika kuanzia Jumanne, zitakuwa za mwaka ujao wa fedha.
LONDON, ENGLAND: DIRISHA hili la usajili linarajia kupamba moto zaidi kwenye klabu za Ligi Kuu England kuanzia wiki hii baada ya awali kuonekana kwenda kwa moto hafifu kwa sababu timu zilikuwa zikisubiri Juni 30 ipite.
Klabu zilikuwa zikisubiri hesabu za kifedha za mwaka uliopita zifungwe, ambapo ilikuwa Jumatatu ya Juni 30 na sasa dili zote zitakazofanyika kuanzia Jumanne, zitakuwa za mwaka ujao wa fedha.
Klabu zitaingia kwenye mwaka mpya wa fedha kwa mujibu wa kanuni za kifedha za Ligi Kuu England, hiyo ikiwa na maana kwamba usajili wowote utakaofanyika kuanzia Julai 1, hesabu zake zitawekwa kwenye akaunti ya msimu wa 2025/26, kuliko dili zilizofanyika kabla ya hapo, ambapo hesabu zake zilikuwa zikiunganishwa kuanzia msimu wa 2024/25.
Hivyo, klabu yoyote iliyokuwa na ukomo kwenye kanuni ya faida na matumizi endelevu (PSR) zingekuwa kwenye wakati mgumu wa kusajili hadi hapo mwaka mpya wa fedha unapoanza.
Klabu zinafahamu wazi kukiuka sera ya PSR matokeo yake ni mabaya, ikiwamo kupokwa pointi, hivyo timu zilikuwa zikivuta muda wa kufanya usajili kabla ya kufikia Juni 30, kuepuka kuongezeka kwa matumizi ambayo yangeingizwa kwenye hesabu za msimu wa 2024/25.
Lakini, sasa dili zote zitakazofanyika kuanzia Jumanne hesabu zitaingizwa kwenye akaunti mpya ya msimu wa 2025/26, ambapo klabu zitakuwa na nafasi kubwa ya kusajili kwa uhuru. Kutokana na hilo, kuna uhakika mkubwa timu zikaanza kuwa bize kusajili kuanzia wiki hii.
Hadi sasa kwenye dirisha hili tayari kumeshuhudiwa uhamisho uliovunja rekodi England baada ya Liverpool kumnasa kiungo wa Kijerumani, Florian Wirtz kwa ada ya Pauni 116.5 milioni, huku miamba hiyo ya Anfield ikitumia karibu Pauni 200 milioni, ikiwamo pia Jeremie Frimpong na Milos Kerkez. Liverpool ilikuwa na jeuri hiyo kwa sababu Liverpool haikufanya usajili kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi, hivyo ilikuwa na fundi la kusajili haraka dirisha hili.
Manchester United ilitumia 62.5 milioni kumsajili Matheus Cunha, lakini huo ni usajili ilioufanya kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi na kinachoelezwa ni kwamba inasubiriwa Julai ifike ili ikamilishe dili jingine, ambapo inamsaka staa wa Brentford, Bryan Mbeumo.
Ofa zao mbili zilikataliwa na Brentford, lakini kuna matumaini makubwa dili litakamilika wiki hii.
Manchester City iliongeza mastaa watatu, Rayan Cherki akiwa miongoni mwao. Kocha wa Man City, Pep Guardiola anataka kujenga kikosi chake mapema na alifanya usajili huo kwa haraka kwa ajili ya fainali za Kombe la Dunia la Klabu, ambapo kikosi hicho kilitarajia kumenyana na Al-Hilal alfajiri ya Jumanne kwenye mchezo wa hatua ya mtoano ya 16 bora.
Newcastle ilibanwa na PSR huko nyuma, lakini sasa ina uwezo wa kusajili. Ilikuwa ikimsaka fowadi wa Brighton, Joao Pedro, lakini wamezidiwa ujanja na Chelsea - hivyo wamebaki kwenye mawindo yao ya kuwasaka kipa James Trafford na winga wa Nottingham Forest, Anthony Elanga.
Arsenal nayo inatarajia kuwa bize kusaka straika kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi na haikufanya uhamisho wowote kabla ya Juni 30, huku kwenye meza yao kukitajwa kuwa na majina ya mastraika matata kabisa, Benjamin Sesko na Viktor Gyokeres.
Haijatangaza pia usajili wa kiungo Martin Zubimendi kutoka Real Sociedad ikisubiri Julai ifike.