Thomas Partey asepa zake Arsenal

Muktasari:
- Staa huyo wa kimataifa wa Ghana, mwenye umri wa miaka 32, alikuwa kwenye mazungumzo ya kusaini dili jipya ili aendelee kubaki Emirates, lakini pande mbili zimeshindwa kufikia makubaliano.
LONDON, ENGLAND: NDO hivyo. Kiungo, Thomas Partey ameondoka kwenye klabu ya Arsenal baada ya mkataba wake kufika ukomo, jana Jumatatu, imeripotiwa.
Staa huyo wa kimataifa wa Ghana, mwenye umri wa miaka 32, alikuwa kwenye mazungumzo ya kusaini dili jipya ili aendelee kubaki Emirates, lakini pande mbili zimeshindwa kufikia makubaliano.
Arsenal sasa itathibitisha kuondoka kwa kiungo huyo muda wowote. Arsenal na Partey walikuwa kwenye mazungumzo ya dili jipya, lakini kwa kipindi hicho kiungo huyo alikuwa huru kuzungumza na klabu za ng’ambo tangu Januari.
Partey alikuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi cha kocha Mikel Arteta kwa msimu wa 2024-25, ambapo alicheza mechi 52 katika michuano yote. Staa huyo wa Black Stars alifunga mabao tisa na kuasisti saba katika mechi 167 alizochezea Arsenal tangu alipojiunga 2020.
Partey alichezeshwa nafasi nyingi na kocha Arteta baada ya Arsenal kuwa na majeruhi wengi msimu uliopita, lakini makubaliano ya kumbakiza yameshindikana na sasa staa huyo ameondoka.
Ukiweka kando kucheza kiungo ya kukaba, Partey alitumika pia kama beki wa kulia msimu uliopita.
Arsenal ipo bize kuboresha safu yake ya kiungo dirisha hili, huku ikielezwa kwamba imeshakamilisha usajili wa staa wa Real Sociedad, Martin Zubimendi. Sambamba na hilo, Arsenal pia ipo kwenye mchakato wa kumsajili nahodha wa Brentford, Christian Norgaard kwa ada ya Pauni 15 milioni. Partey alinaswa kwa ada ya Pauni 42.7 milioni akitokea Atletico Madrid.