Rashford, Barcelona sasa mambo freshi!
Muktasari:
- Baada ya kuridhishwa na mchango wake kiwanjani na kuendana na falsafa ya timu, uongozi wa Barca umechukua hatua ya kumalizia dili hilo ili kumbakisha nyota huyo Camp Nou kwa muda mrefu.
BARCELONA imefikia makubaliano ya kumsainisha mkataba wa moja kwa moja mshambuliaji wa Manchester United na timu ya taifa ya England, Marcus Rashford, 28, anayecheza katika kikosi chao kwa mkopo wa msimu mmoja.
Baada ya kuridhishwa na mchango wake kiwanjani na kuendana na falsafa ya timu, uongozi wa Barca umechukua hatua ya kumalizia dili hilo ili kumbakisha nyota huyo Camp Nou kwa muda mrefu.
Barca italazimika kutoa Euro 30 milioni kama ada ya uhamisho ya kukamilisha dili hilo kiasi ambacho hawaoni kama ni kikubwa sana kwao ukilinganisha na hali ya soko ilivyo kwa sasa ambapo mshambuliaji aina ya Rashford ingehitajika zaidi ya Euro 60 milioni ili kumpata.
Inaelezwa kocha Hansi Flick, ndiye aliyechangia sana uamuzi huo kufanyika mapema kwani mara zote ameweka wazi kwamba anavutiwa na mchango ambao staa huyo ameuonyesha tangu ajiunge katika timu yake ambapo licha ya kuwa mgeni haijamchukua muda mrefu kuendana na falsafa ya timu.
Mabosi wa Barca walikaa kikao cha mwisho katika ofisi za timu hiyo wiki iliyopita ambapo wakafikia uamuzi wa kutoa fungu la usajili huo. Mkataba wa Rashford na Man U unaisha 2028 na tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi 32, amefunga mabao 10 na kutoa asisti 13.
Rodri
REAL Madrid imeongeza kasi katika harakati za kumfuatilia kiungo wa Manchester City, Rodri, 29, ambaye mkataba wake wa sasa na Man City unatarajiwa kumalizika mwaka 2027.
Madrid inamwona Rodri kama chaguo bora la kuimarisha safu ya kiungo kutokana na uzoefu wake licha ya kufahamu kwamba itakuwa ngumu kumpata kutokana na umuhimu wake katika kikosi cha Man City.
Hata hivyo, hali yake ya mkataba ndiyo inayowapa matumaini zaidi ya kuona dili hilo linaweza kufanikiwa.
Leon Goretzka
ARSENAL bado ina nia kubwa ya kumsajili kiungo wa Bayern Munich, Leon Goretzka, 31, kwa uhamisho wa bure katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Inaelezwa kuwa The Gunners walijaribu kumsajili staa huyo Januari, lakini dili hilo halikufanikiwa, hivyo sasa wanapanga kurejea tena mwisho wa msimu ambapo mkataba utakuwa umeisha.
Akiwa na Bayern msimu huu, staa huyu wa kimataifa wa Ujerumani amecheza mechi 18 za michuano yote.
Dusan Vlahovic
JUVENTUS haijafanya mazungumzo yoyote ya kumuongeza mkataba mshambuliaji wao Dusan Vlahovic, 26, tangu dirisha lililopita la majira ya kiangazi licha ya mkataba wake kuelekea ukingoni.
Kutokana na hali hiyo, vigogo kadhaa wameonyesha nia ya kumsajili ikiwamo Chelsea, Tottenham Hotspur, AC Milan, Inter Milan na Roma. Vlahovic anaendelea kuwa mmoja wa washambuliaji wanaowindwa zaidi barani Ulaya.
Michael Kayode
MANCHESTER United na Newcastle United zimeingia katika orodha ya klabu zinazomfuatilia beki wa kulia wa Brentford na timu ya taifa ya vijana ya Italia, Michael Kayode, 21. Kayode ambaye alijiunga na Brentford mwaka jana amekuwa bora sana katika EPL kwa msimu huu na hiyo imefanya timu nyingi kummezea mate. Kwa mujibu wa vyanzo vya ndani, Kayonde mwenyewe hana presha licha ya kuhusishwa na vigogo hao.
Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2030.
Paulo Dybala
ROMA imewaambia nyota wao Paulo Dybala, 32, na Lorenzo Pellegrini, 29, kuwa watatakiwa kukubali kupunguziwa mshahara ikiwa wanahitaji kuendelea kusalia katika timu hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa, wachezaji hao watalazimika kupunguza mishahara yao kwa sababu mikataba yao baada ya mikataba yao inayomalizika mwisho wa msimu kuisha. Uongozi wa Roma unapambana kwa ajili ya kujikwamua katika hali mbaya ya kiuchumi.
Sandro Tonali
KIUNGO wa kimataifa wa Italia, Sandro Tonali, 25, anaweza kuomba kuondoka Newcastle United ikiwa klabu hiyo itashindwa kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
Tonali amekuwa akihusishwa na klabu kubwa barani Ulaya, lakini amesita kufanya uamuzi yoyote hadi msimu utakapomalizika ili aone ikiwa Newcastle itafuzu Uefa au laa na ikishindwa ndio ataomba kuondoka.
Arsenal ni miongoni mwa timu zinazohitaji saini ya fundi huyu na ipo tayari kulipa hadi Pauni 50 milioni ili kukamilisha dili lake.
Denzel Dumfries
LIVERPOOL imeanza kufanya tena mawasiliano na wawakilishi wa beki wa pembeni wa Inter Milan na timu ya taifa ya Uholanzi, Denzel Dumfries mwenye umri wa miaka 29, ili kumsajili staa huyo katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Dumfries amekuwa mhimili muhimu katika kikosi cha Inter kutokana na nguvu, kasi na uwezo wake wa kusaidia mashambulizi. Liverpool inapambana kuimarisha maeneo ya pembeni.