Rashford ana masharti 10 Barcelona
Muktasari:
- Kocha Hansi Flick amekuwa kwenye kikosi cha Barca kwa mwaka sasa na kukiongoza kubeba mataji yote matatu ndani ya Hispania msimu uliopita, ambapo ni La Liga na makombe mengine mawili ya ndani.
BARCELONA, HISPANIAL: SUPASTAA, Marcus Rashford anakaribia kukamilisha uhamisho wake wa kujiunga na Barcelona lakini ili kwenda kufanikiwa huko, itamlazimu kufuata sheria hizi 10.
Kocha Hansi Flick amekuwa kwenye kikosi cha Barca kwa mwaka sasa na kukiongoza kubeba mataji yote matatu ndani ya Hispania msimu uliopita, ambapo ni La Liga na makombe mengine mawili ya ndani.
Lakini, kufikia mafanikio hayo ameweka sheria zake zinazopaswa kufuatwa na wachezaji ikiwamo kuwahi mazoezini dakika 90 kabla ya kuyajaanza.
Kwa mujibu wa Gazeti la AS, hiyo ni moja ya sheria 10 za Flick, ambazo mastaa wa Barca wanaiishi, hivyo Rashford anapaswa kuzoea hilo haraka kama anataka kutoboa Camp Nou. Kingine itambidi kuzoea mazoezi magumu ya Flick, ambaye amekuwa akifanya vipindi vyake vya mazoezi kwa dakika 90.
Kwenye kila siku ya mechi kutakuwa na vipindi vya mazoezi asubuhi, kisha sheria nyingine za kocha huyo ni kuhakikisha wachezaji wote wanakutana hotelini kabla ya mechi kwa sababu hataki kukutana na sapraizi yoyote. Mapumziko ni siku moja tu kwa wiki kwa sababu kocha Flick anataka muda wote awe na wachezaji wake.
Kocha Flick anafahamu wazi kila mchezaji anajitambua, hivyo hajaweka faini zozote kwa wachezaji, huku akitaka kila mmoja kula chakula kilichoandaliwa na mpishi wao, Silvia Tremoleda kwenye kantini ya klabu Ciutat Esportiva.
Na wachezaji wa Barca wanapaswa kupima uzito kila siku ili kujiweka fiti na katika kuwafanya wanakuwa fiti muda wote, kocha huyo amepiga marufuku ndege za usiku baada ya mechi za ugenini, kitu ambacho Rashford anapaswa kutambua.
Staa huyo wa England amekubali uhamisho wa mkopo kwenda Barca wenye kipengele cha kubebwa jumla mwisho wa msimu endapo kama ataonyesha kiwango bora.