Rashford aikataa Man United, akubali kukatwa mshahara
Muktasari:
- Rashford, 28, anaonekana kuwa na nia ya kubaki Barcelona, kiasi cha kuwa tayari kukubali kupunguzwa kwa kiasi kikubwa cha mshahara wake.
BARCELONA, HISPANIA: MSHAMBULIAJI wa Manchester United, Marcus Rashford ameripotiwa kuwa tayari kupunguza mshahara wake ili kukamilisha usajili wake wa kujiunga moja kwa moja na maimba ya soka la Hispania, Barcelona anayoichezea kwa mkopo.
Taarifa kutoka vyombo vya habari vya Hispania zinaeleza Rashford hana mpango wa kurejea Manchester United tena, licha ya kuwa bado ana mkataba unaoendelea hadi mwaka 2028.
Inadaiwa Barcelona wanataka kupunguza ada ya uhamisho ambayo awali ilikubaliwa kuwa Pauni 25 milioni, jambo linaloweza kuhatarisha dili hilo kukamilika.
Rashford, 28, anaonekana kuwa na nia ya kubaki Barcelona, kiasi cha kuwa tayari kukubali kupunguzwa kwa kiasi kikubwa cha mshahara wake.
Msimu huu, Rashford amefunga mabao 13 na kutoa pasi 11 za mabao katika mashindano yote huku pia akichangia kupatikana kwa penalti mbili.
Kiwango chake kimekuwa bora, amekuwa akihusika katika bao kila baada ya dakika 89, takwimu inayomfanya kuwa mmoja wa wachezaji bora katika ligi hiyo.
Licha ya kuanza katika mechi chache kutokana na ushindani mkubwa wa washambuliaji ndani ya kikosi cha Barcelona, Rashford hajachukulia hali hiyo kama tatizo.
Kocha wa Barcelona, Hansi Flick ameeleza kuridhishwa na mchango wa Rashford, ingawa hakutaka kuzungumzia hatma yake kwa sasa.
Kwa upande wa Manchester United, kurejea kwa Rashford kunaweza kuongeza mzigo wa mishahara, hasa wakati klabu hiyo ikijaribu kupunguza matumizi chini ya uongozi wa Jim Ratcliffe.