Rashford aibua wasiwasi Barca
Muktasari:
- Fowadi huyo wa Manchester United, Rashford, 27, alitua Hispania kukamilisha uhamisho wake wa mkopo wa msimu mzima kwenye kikosi hicho cha Camp Nou huku kukiwa na kipengele cha kumchukua jumla mwishoni mwa msimu.
BARCELONA, HISPANIA: SUPASTAA, Marcus Rashford huenda akashindwa kuichezea Barcelona hata baada ya kujiunga na miamba hiyo ya LaLiga.
Fowadi huyo wa Manchester United, Rashford, 27, alitua Hispania kukamilisha uhamisho wake wa mkopo wa msimu mzima kwenye kikosi hicho cha Camp Nou huku kukiwa na kipengele cha kumchukua jumla mwishoni mwa msimu.
Kinachoaminika alifanya vipimo vya afya Jumatatu na alitarajia kuungana na wenzake mazoezini Jumanne kabla ya utambulisho wake rasmi Jumatano.
Lakini, Rashford bado haelewi kama atachezea timu hiyo kwa haraka kutokana na ishu yake ya kuandikishwa kwenye La Liga.
Kwa mujibu wa Mark McAdam wa Sky Sports, miamba hiyo ya La Liga kwa sasa haitakuwa na uwezo wa kumwandikisha Rashford kwenye La Liga, hivyo itahitaji kupunguza wachezaji kwanza ili kupata nafasi hiyo.
Kabla ya vipimo vya afya vya Rashford, Andy Brassell wa talkSPORT alisema matatizo ya kifedha ya Barcelona yanaweza kuchelewesha kwa muda staa huyo wa England kuandikishwa kwenye La Liga ili aanze kutumiwa na miamba hiyo.
Brassell alisema: “Hakuna uhakika, kama unavyojua rais wa La Liga, Javier Tebas, Barcelona inaweza kumwandikisha Rashford kwa muda huu tu. Hicho kitu kinapaswa kufuatiliwa kuhusu usajili wa Barcelona. Walijiondoa kwenye dili la Nico Williams.
“Rashford hakunaswa kwa pesa nyingi, lakini kuna ishu ya mshahara wake.”
Barcelona imekumbwa na sakata la kufika ukomo wa matumizi kwenye La Liga kwa miaka ya hivi karibuni, kitu ambacho kilichelewesha uandikishwaji wa wachezaji Dani Olmo na Pau Victor msimu uliopita. Bosi wa LaLiga, Javier Tebas alifichua kwamba hali ya kifedha ya klabu hiyo ndiyo iliyotibua dili la Nico Williams, ambaye aliamua kusaini dili jipya la kubaki Athletic Bilbao.