Rais wa soka Asia aunga mkono ratiba ya Kombe la Dunia 2034
Muktasari:
- Sheikh Salman ameeleza kwamba, ratiba ya majira ya baridi huleta ubora zaidi wa michezo, kwani wachezaji huwa katikati ya msimu wao wa ligi, hasa wale wanaocheza Ulaya.
Kwa kuwa fainali za Kombe la Dunia zinatarajiwa kurejea barani Asia miaka 12 baada ya kufanyika Qatar, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Asia (AFC), Sheikh Salman bin Ebrahim Al Khalifa anaamini bara hilo linaweza kuwa chaguo sahihi kwa mashindano hayo makubwa ya mpira wa miguu duniani.
Kuna uwezekano mkubwa kwamba, kama ilivyokuwa kwenye fainali za Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar, mwaka 2034 nchini Saudi Arabia pia zitachezwa katika miezi ya baridi ili kuepuka joto kali la kiangazi. Ingawa uamuzi wa mwisho bado haujafikiwa, wazo hilo limeungwa mkono na Rais wa AFC.
FIFA ilithibitisha mwishoni mwa mwaka jana kwamba Saudi Arabia itatimiza ndoto yake ya muda mrefu ya kuandaa mashindano hayo makubwa ya soka duniani baada ya kupata uenyeji bila kupingwa, na hivyo kuwa nchi ya pili katika Rasi ya Arabia kuandaa Kombe la Dunia baada ya Qatar. Kombe la Dunia la Qatar lilifanyika kwa mara ya kwanza mwezi Novemba hadi Desemba 2022 ili kuepuka joto kali la jangwani, na Sheikh Salman anapendekeza Wasaudi wafanye vivyo hivyo.
“Sioni kama kuna njia nyingine, lakini bado kuna muda mrefu hadi 2034, lakini itategemea FIFA na mashirikisho mengine kufikia uamuzi,” Sheikh Salman, ambaye pia ni makamu wa rais wa FIFA, ameliambia gazeti la Dawn wakati wa ziara yake ya siku tatu nchini Pakistan kama mgeni wa serikali.
“Wakati ukifika wataamua, lakini mimi nakubaliana kwamba Kombe la Dunia halipaswi kuwa wakati wa kiangazi pekee,” ameongeza.
“Hata Marekani, ambao ni wenyeji wa Kombe la Dunia 2026 pamoja na Canada na Mexico, wakati wa majira ya kiangazi joto ni kali katika baadhi ya miji na kucheza mechi mchana ni vigumu kwa wachezaji.”
Sheikh Salman ameeleza kwamba, ratiba ya majira ya baridi huleta ubora zaidi wa michezo, kwani wachezaji huwa katikati ya msimu wao wa ligi, hasa wale wanaocheza Ulaya.
“Watu watasema ratiba inavuruga kalenda ya soka, lakini unapokuwa na wachezaji walioko kwenye kiwango kizuri cha msimu, unaona tofauti uwanjani,” amesema, akitolea mfano Lionel Messi, ambaye aliiongoza Argentina kutwaa Kombe la Dunia 2022 kwa kiwango bora.
“Sidhani kama mchezaji kama Messi angeweza kucheza vizuri katika umri wake kama angekuwa amemaliza msimu mzima na kucheza majira ya kiangazi. Alikuwa bora kabisa, alishinda tuzo ya mchezaji bora, na sote tunakubaliana alistahili.”
Sheikh Salman pia amesifu Qatar kwa kuandaa Kombe la Dunia bora bila matatizo yoyote.
“Sidhani kama Qatar walipata sifa waliyostahili kutokana na mafanikio yao,” amesema.
“Wengi, hasa katika mataifa ya Magharibi, hawakutaka kusema mazuri kuhusu jinsi Waqatar walivyoshughulikia mashindano hayo. Lakini kwangu mimi, lilikuwa Kombe la Dunia bora zaidi tangu niwe kwenye soka. Nilikuwepo, niliona viwanja, na niliona jinsi timu zilivyokuwa zinarudi hotelini ndani ya saa moja baada ya mechi.”
Kombe la Dunia la Qatar lilikuwa la mwisho kushirikisha timu 32, huku toleo la mwaka 2026 likiwa la kwanza kushirikisha timu 48. Kumekuwa na mazungumzo kuhusu kuongeza idadi hiyo hadi timu 64 kwa Kombe la Dunia la 2030, litakalofanyika Hispania, Ureno, na Morocco, huku baadhi ya mechi zikifanyika Amerika Kusini.
Mwezi Aprili 2025, waziri wa michezo wa Saudi Arabia, Prince Abdelaziz Turki bin Faisal, alisema nchi yake iko tayari kuandaa hata Kombe la Dunia lenye timu nyingi zaidi, lakini Sheikh Salman anasema ni mapema mno kufanya uamuzi huo.
“Sipingani na kuwa na timu 64,” amesema.
“Lakini sipendi kubadili kanuni zilizopitishwa. Tayari FIFA imeamua kuhusu timu 48 kwenye mikutano yake, na zabuni za uenyeji kwa 2026, 2030, na 2034 ziliidhinishwa kwa msingi huo. Nchi mwenyeji ina wajibu wa kutimiza mahitaji yote kama viwanja, kambi za mazoezi, na gharama zinazohusiana.
“Hatujajaribu mfumo wa timu 48 bado. Tutaona matokeo yake kwenye Kombe la Dunia mwaka 2026. Tukishaona kama ni mafanikio au la, ndipo tutaamua kama tuongeze, tubaki pale pale, au tupunguze. Itategemea kilicho bora kwa FIFA na wanachama wake 211.”
Hata hivyo, msukumo wa kuongeza idadi ya timu unaendelea, kwa lengo la kupanua ushiriki na mashabiki duniani kote. Lakini upanuzi huo unaleta changamoto, hasa kwa mataifa yanayoweza kuandaa mashindano makubwa kama hayo.
Kwa kuwa fainali za Kombe la Dunia zitarudi barani Asia miaka 12 baada ya kufanyika Qatar, Sheikh Salman anaamini bara hilo linaweza kuwa kitovu cha soka duniani siku zijazo.
“Nadhani Asia ni bara la pili lenye uwezo wa kuandaa Kombe la Dunia mara kwa mara,” amesema.
“Tunajua Ulaya ina miundombinu bora, lakini kutokana na upanuzi wa mashindano haya, si rahisi kwa nchi kuandaa kwa gharama na miundombinu inayohitajika. Tumeona Qatar walivyofanya vizuri mwaka 2022, na inaweza kuwa vigumu kurudia mafanikio hayo na timu 32. Labda siku zijazo tutarudi kwenye timu 32, lakini hilo halijulikani bado.”