Rais FIFA aipongeza Black Stars kufuzu Kombe la Dunia 2026
Muktasari:
- Ghana imepata nafasi ya kuwa miongoni mwa timu za Afrika zitakazoshiriki fainali hizo, baada ya kuifunga Comoro bao 1-0, katika mechi yamwisho ya kundi I, iliyochezwa kwenye Uwanja wa Accra jana Jumapili Oktoba 12, 2025. Bao lilifungwa na kiungo mshambuliaji wa Totenham, Mohammed Kudus.
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kimataifa (FIFA), Gianni Infantino, ametuma salamu za pongezi kwa timu ya taifa ya Ghana maarufu Black Stars, kufuatia kufuzu fainali za Kombe la Dunia la FIFA 2026 zitakazofanyika Canada, Mexico, na Marekani.
Ghana imepata nafasi ya kuwa miongoni mwa timu za Afrika zitakazoshiriki fainali hizo, baada ya kuifunga Comoro bao 1-0, katika mechi yamwisho ya kundi I, iliyochezwa kwenye Uwanja wa Accra jana Jumapili Oktoba 12, 2025. Bao lilifungwa na kiungo mshambuliaji wa Totenham, Mohammed Kudus.
Katika taarifa yake iliyotumwa kwenye Chama cha Mpira wa Miguu Ghana (GFA), Infantino amepongeza juhudi, nidhamu, na ari ya wachezaji wa Black Stars katika kuiwakilisha nchi hiyo kwenye mapambano ya kufuzu fainali za Kombe la Dunia.
"Hongera kwa Black Stars kufuzu fainali za Kombe la Dunia kwa mara ya tano katika historia.
"Mashabiki wenu wataongeza rangi, mtindo, na shauku katika fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwaka 2026, na tunatarajia timu yenu kuibua nyota wengine wa kimataifa kama ilivyokuwa kwa kikosi maarufu kilichofika robo fainali ya michuano hiyo huko Afrika Kusini mwaka 2010," imeeleza taarifa ya Infantino.
Ujumbe huo kutoka kwa kiongozi huyo wa juu wa FIFA, umeongeza hamasa kwa Black Stars, ambao wamefanya kazi kwa bidii kuhakikisha nafasi yao kwenye michuano hiyo mikubwa.
Kufuzu kwao ni ushahidi wa maendeleo ya mpira wa miguu nchini Ghana, na taifa hilo linaisubiri kwa hamu fursa ya kuwaona mashujaa wao wakionesha makali yao kimataifa.
Ghana imeongoza kundi I kwa kufikisha pointi 25, ikifuatiwa na Madagascar yenye pointi 19, huku ikishika nafasi ya tatu kwa kuwa na pointi 18.
Comoro imeshika nafasi ya nne ikiwa na pointi 15, ikifuatiwa na Jamhuri ya Afrika ya kati yenye pointi 08 na chad inaburuza mkia wa kundi hilo kwa kuwa na pointi 1.
Droo ya mwisho ya kupanga makundi ya Kombe la Dunia inatarajiwa kufanyika Desemba 5, 2025, na Infantino ameeleza kuwa na shauku ya kujua Ghana itakutana na timu zipi kwenye mashindano hayo.
Kwa mashabiki wao na wachezaji wenye vipaji, Ghana bila shaka itaacha alama kubwa kwenye Kombe la Dunia la 2026.
Kabla ya 2026, Ghana tayari imewahi kushiriki michuano ya Kombe la Dunia la FIFA mara nne, katika miaka ya 2006, 2010, 2014 na 2022. Mwaka 2006, ilikuwa timu pekee kutoka Afrika iliyofanikiwa kufika hatua ya mtoano nchini Ujerumani, na ikawa taifa la sita mfululizo kutoka Afrika kuvuka hatua ya makundi katika michuano ya Kombe la Dunia.