Raiola atibua dili la Haaland Madrid

Raiola atibua dili la Haaland Madrid

Muktasari:

  • REAL Madrid imepoteza matumaini na wakala maarufu wa wanasoka Mino Raiola na sasa imeanza kujifikiria upya juu ya mpango wao wa kumsajili straika, Erling Haaland, imeripotiwa.

REAL Madrid imepoteza matumaini na wakala maarufu wa wanasoka Mino Raiola na sasa imeanza kujifikiria upya juu ya mpango wao wa kumsajili straika, Erling Haaland, imeripotiwa.

Straika, Haaland amekuwa akizivutia klabu nyingi kwelikweli za kiwango cha juu huko Ulaya baada ya kufunga mabao 33 katika mechi 32 za michuano yote aliyochezea Borussia Dortmund msimu huu.

Mabao hayo, amefunga kwenye kikosi cha Dortmund ambacho kwa sasa hakipo kwenye ubora wake na kujiweka kwenye hatari ya kukosekana katika Top Four ya Bundesliga na kama hilo likitokea na kushindwa kukamatia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao basi anaweza kuachana na maisha ya Signal Iduna Park mwishoni mwa msimu huu.

Wakala Raiola alipiga safari za kuzunguka Ulaya kwenda kukutana na timu kadhaa ikiwamo Barcelona na Real Madrid kwa ajili ya kumchukua mchezaji huyo, lakini kinachoelezwa ni kwmaba alipoteza tu muda wake kwenda Madrid. Kinachoelezwa ni kwamba Los Blancos wanajifikiria mara mbili kuhusu ishu ya Haaland baada ya dili za miaka ya nyuma walizofanya na Raiola.

Real Madrid ilijaribu kuwasajili wateja wengine wawili wa Raiola, Paul Pogba na Gianluigi Donnarumma, lakini walishindwa kukamilisha dili hizo kutokana na cha juu kikubwa alichokuwa akitaka kulipwa wakala huyo.

Licha ya Haaland kuwa mmoja wa mastaa moto kabisa Ulaya kwa sasa, lakini dili hizo zilizotangulia na pesa alizokuwa akitaka kulipwa Raiola zinaifanya Real Madrid kufikiria kufanya usajili wa mastaa wengine.

Jambo hilo litaifanya Barcelona kuwa timu pekee yenye nafasi kubwa ya kumnasa Haaland huko Hispania, huku miamba hiyo ya Nou Camp ikiamini usajili wa straika huyo unaweza kumshawishi Lionel Messi akabaki kwenye kikosi chao. Messi mkataba wake utafika tamati mwishoni mwa msimu huu na bado hakuna mazugumzo mapya.

Real Madrid sasa wameelekeza nguvu yao kwenda usajili wa supastaa wa Paris Saint-Germain, Kylian Mbappe.