Raia nusura wamuue mkongwe kwa ujambazi
Muktasari:
- Lara aliyezichezea timu mbalimbali Amerika na Asia, enzi zake uwanjani anakumbukwa kwa kuichezea nchi hiyo kwenye fainali za Kombe la Dunia 2006, ambako alifunga moja ya mabao katika mechi za kufuzu dhidi Argentina.
QUITO, ECUADOR: MCHEZAJI maarufu wa zamani wa Ecuador, Christian Lara, amekamatwa kwa tuhuma za kuhusika katika jaribio la ujambazi wa kutumia silaha, na kushambuliwa na wananchi waliokuwa jirani na eneo alilokuwa akifanyia uharifu.
Lara aliyezichezea timu mbalimbali Amerika na Asia, enzi zake uwanjani anakumbukwa kwa kuichezea nchi hiyo kwenye fainali za Kombe la Dunia 2006, ambako alifunga moja ya mabao katika mechi za kufuzu dhidi Argentina.
Picha za video zilizosambazwa mitandaoni na kwenye televisheni zilimuonyesha mchezaji huyo akipigwa ngumi na mateke na watu waliokuwa na hasira kabla ya polisi kufika na kumunusuru kwa kumuingiza kwenye gari lao la doria.
Lara, mwenye umri wa miaka 45 na anayejulikana kwa jina la utani “Diablito” kutokana na kimo chake cha futi 5 na inchi 2, alionekana akiwa amevaa suruali nyeusi na koti lenye rangi nyekundu na nyeusi.
Kwa mujibu wa polisi, watu wanne kati ya sita waliodaiwa kuhusika na jaribio la ujambazi walikamatwa, ambapo mkuu wa polisi Pablo Lastra amesema watuhumiwa hao walikuwa wanajaribu kuvamia duka la vifaa vya elektroniki katika kitongoji cha La Magdalena jijini Quito.
Polisi wamesema walikamata silaha tatu zikiwemo bunduki zilizotengenezwa kienyeji pamoja na risasi na bidhaa za kielektroniki. Lara alikamatwa ndani ya gari lililokuwa likisubiri nje ya duka akidaiwa kuwa ndiye aliyekuwa dereva wa gari la kutorokea.
Lara aliwahi kuwa mchezaji muhimu wa Ecuador, na pia kucheza ligi za nje ikiwemo Qatar, Colombia na Mexico. Alicheza mechi 28 za timu ya taifa akiisaidia Ecuador kufuzu Kombe la Dunia 2006 baada ya kuifunga Argentina 2–0 katika mechi ya kufuzu. Kwa sasa, waendesha mashtaka wanaendelea na uchunguzi ili kubaini iwapo Lara atafunguliwa mashtaka.