Rafiki ampa ushauri wa bure Pep Guardiola
Muktasari:
- Planchart, ambaye aliwahi kuwa mchambuzi viwango vya wachezaji, amesema Guardiola anapaswa kuchukua mapumziko ili kujitengeneza upya na baada ya hapo atafute timu nyingine ya kuifundisha.
MANCHESTER, ENGLAND: MKUFUNZI Carles Planchart ambaye ni miongoni mwa watu wanaoaminiwa sana na Pep Guardiola amemshauri kocha huyo kuondoka Manchester City mwisho wa msimu huu.
Planchart, ambaye aliwahi kuwa mchambuzi viwango vya wachezaji, amesema Guardiola anapaswa kuchukua mapumziko ili kujitengeneza upya na baada ya hapo atafute timu nyingine ya kuifundisha.
Wawili hao walifanya kazi pamoja Barcelona, Bayern Munich na Manchester City kabla ya Planchart kuondoka katika nafasi yake msimu uliopita.
Fundi huyu ambaye amefanya kazi na Guardiola kwa miaka 18, anaamini kocha huyo anahitaji kupumzika kwa muda ikiwa anataka kuendelea na kazi yake ya ukocha kwa muda mrefu.
Mkataba wa Guardiola na Man City unamalizika mwaka 2027, na tayari amewahi kusema kuwa anatala kupumzika kwa muda baada ya kuondoka viunga vya Etihad Stadium.
"Kuendelea kubakia pale hadi sasa ni uamuzi wake binafsi. Nafikiri kocha anatakiwa kuwa katika kwa miaka mitano au sita, si zaidi," amesema Planchart alipokuwa anafanya mazungumzo na gazeti la SPORT.
"Hii sio kwake tu, hata kwa mtu mwingine yoyote, Baada ya kudumu katika timu kwa miaka sita, unapaswa kuacha na kupumzika ili kupata muda wa kurudi upya. Kama rafiki, ningemshauri aondoke, apumzike kisha atafute timu mpya kwa sababu bado ana safari ndefu mbele. Najua amekuwa Man City kwa muda mrefu kwa sababu mabosi walituchukulia kama familia, wametupa uhuru wa kufanya kazi kama nyumbani. Haikuwa hivyo Barcelona wala Bayern."
Planchart pia ameeleza kuwa sababu ya Man City kwa sasa kutokuwa katika ubora uliozoeleka ni matatizo mengi yanayoikumba ikiwemo majeruhi, baadhi ya wachezaji kuondoka na benchi la ufundi kuishiwa nguvu baada ya mapambano ya muda mrefu.
"Kulikuwa na kushuka kwa utendaji, hata kwa benchi la ufundi. Hiyo ilisababisha tupambane tu walau kupata nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa, na hilo lilikuwa ni jambo la mafanikio kwa msimu uliopita."