Magwiji Man United wampa onyo Amorim
Muktasari:
- Kocha huyo Mreno amesisitiza baada ya kichapo cha mabao 3-0 kutoka kwa watani wao wa jadi Manchester City uwanjani Etihad, Jumapili iliyopita kwamba ataendelea kutumia mtindo wake wa kiuchezaji wa fomesheni ya 3-4-2-1.
MANCHESTER, ENGLAND: RUBEN Amorim ameambiwa aache kuwa kichwa ngumu na badala yake abadilishe staili ya uchezaji kama anataka kuendelea kubaki kwenye kibarua cha kuinoa Manchester United.
Kocha huyo Mreno amesisitiza baada ya kichapo cha mabao 3-0 kutoka kwa watani wao wa jadi Manchester City uwanjani Etihad, Jumapili iliyopita kwamba ataendelea kutumia mtindo wake wa kiuchezaji wa fomesheni ya 3-4-2-1.
Kipigo hicho kutoka kwa Man City kimeifanya Man United kuwa na mwanzo wa hovyo kwenye Ligi Kuu England tangu mwaka 1992 baada ya kukusanya pointi nne katika mechi nne.
Mastaa wawili wa Man United wa kizazi cha ‘Class of ‘92’, Paul Scholes na Nicky Butt, wamesema kocha huyo wa zamani wa Sporting Lisbon anapaswa kufanya uamuzi wa haraka.
Mastaa hao wawili wanaamini kocha wa sasa ameifanya Man Unitd kuwa nyepesi sana kukabiliana nayo na kama hatabadilika basi kufukuzwa kutamuhusu.
Hata hivyo, si kocha tu anayebebeshwa lawama, kiungo wa shoka, Butt alisema wachezaji wa sasa wa Man United wapo kama maroboti na kuamini kwamba kuna kitu hakipo sawa Old Trafford.
Amorim amekuwa kwenye presha kubwa kuhusu kibarua chake na Butt amesema: “Achana na mfumo kwanza, wachezaji wenyewe viwango vyao havipo kwenye ubora unaohitajika, hawapo shapu na hawapambani vya kutosha.
“Viungo wawili, Bruno Fernandes na Manuel Ugarte, hawakuwa na nguvu ya kupambana na watu watatu kwenye eneo la kati. Kama anataka kupata matokeo na kuokoa kibarua chake kidumu muda mrefu, anapaswa kuacha msimamo wa ajabu, abadilike, la ataendelea kupoteza mechi.
“Mtazame Pep Guardiola amekuwa na falsafa ya mpira ambayo kila mtu anapenda kuiona hasa mashabiki wa Man United. Lakini, amebadilika. Amemtoa Jeremy Doku kushoto na kumtumia katikati, kwa sababu kila mtu anajua namna Man United inavyocheza.”
Mchezaji mwenzake Butt wa zamani huko Old Trafford, kiungo matata, Scholes alisema kitendo cha Amorim kukataa kubadilika hilo litamweka kwenye urahisi wa mabosi kumfuta kazi.
Amesema: “Unazungumzia falsafa zake, staili yake ya uchezaji na anavyotaka timu icheze. Kuna makocha wengi sana wajanja England na duniani, wanaweza kukabiliana na staili yake kirahisi sana. Wanafahamu Man United itakwenda kuchezaje kila wiki.
“Majina ya kikosi yanapotangazwa saa moja kabla ya mechi, wapinzani watakuwa wanafahamu jinsi wapinzani wao watakavyokwenda kucheza. Kwa staili ya Amorim anayotaka, kila mtu atakuwa anajua wanavyocheza, hivyo itakuwa kazi rahisi kwa makocha wa upinzani na yeyote kwenye Ligi Kuu England anaweza kutufunga.”
Hata hivyo, Scholes hana uhakika kama kikosi hicho kitabadili mambo na kuanza kufanya vizuri hata kama Amorim atabadili staili yake ya uchezaji na kurudi kwenye mtindo wa zamani.
Amesema: “Sina uhakika, hata kama atabadilika na kucheza 4-3-3, wachezaji wana uwezo wa kutosha? Kipindi chetu, kulikuwa na wachezaji wengi sana wazoefu, ilikaribia hatua hata kocha alikuwa hahitajiki. Kwa sasa hakuna anayechukua majukumu, wachezaji wenye uzoefu wapo, lakini hayupo anayesimama mstari wa mbele kujivika majukumu.”
Butt aliongeza: “Wapo kama maroboti.”
Scholes pia alikosoa usajili wa timu hiyo, akidai wahusika kwenye kufanya usajili Jason Wilcox na Omar Berrada, wametumia pesa nyingi kufanya usajili wa wachezaji wa kawaida.
“Imesajili namba 10 wawili, Matheus Cunha na Bryan Mbeumo na hapo hapo tayari yupo Mason Mount. Ona tulihitaji kipa wa kiwango cha dunia na kiungo wa kukaba, wote hawakusajiliwa.”
Man United iliamua kuachana na mpango wa kumsajili kipa Emi Martinez kwenye siku ya mwisho ya kufungwa kwa dirisha la usajili, ikaenda kumsajili kinda Senne Lammens.
Scholes anashangaa kwa nini timu hiyo haijafanya usajili wa kipa Gianluigi Donnarummana na kumwaacha aende Man City, akiliita hilo ni kosa la jinai.