Pep Guardiola amaliza utata ishu ya Erling Haaland
Muktasari:
- Mshambuliaji huyo wa Norway amefunga mabao 11 katika mechi nane tangu kuanza kwa msimu huu na bado ana mkataba mrefu wa kuwatumikia matajiri hao wa Jiji la London.
MANCHESTER, ENGLAND: KOCHA wa Manchester City, Pep Guardiola amezima uvumi unaomhusisha Erling Haaland na kuhamia Barcelona, akisisitiza kuwa mshambuliaji huyo “sio mjinga” kiasi cha kutaka kuondoka Manchester City baada ya kusaini mkataba wa miaka kumi.
Mshambuliaji huyo wa Norway amefunga mabao 11 katika mechi nane tangu kuanza kwa msimu huu na bado ana mkataba mrefu wa kuwatumikia matajiri hao wa Jiji la London.
Hivi karibuni zilitoka taarifa kwamba rais wa Barcelona, Joan Laporta, amemweka Haaland kwenye orodha yake ya wachezaji atakaoahidi kuwasajili mwakani kama sehemu ya kampeni yake ya uchaguzi ujao.
Mabingwa hao kutoka Catalonia wanadaiwa kuwa na ndoto ya kumsajili Haaland, mwenye umri wa miaka 25, na kizazi chao kijacho cha nyota, ili akaunde safu hatari ya ushambuliaji akishirikiana na mastaa wengine wa Barca kama Lamine Yamal na Pedri.
Hata hivyo, uwezekano wa kumpata unaonekana kuwa mgumu kutokana na mkataba wake ambao unatarajiwa kumalizika mwaka 2034, na ili kuuvunja itahitaji kiasi kikubwa sana cha pesa ambacho kwa Barca sasa ni ngumu kukitoa kutokana na hali yao ya kiuchumi.
Alipoulizwa kuhusu uvumi wa kuondoka, Guardiola amesema: “Nadhani Erling sio mjinga kiasi cha kusaini mkataba hivi karibuni halafu anajua kwamba anataka kuondoka, hawezi kufanya hivyo, lakini mwisho wa yote ni soka nani ajuaye kinachotokea kesho. Hakuna anayejua. Mimi sijui kitakachotokea. Najua ana mkataba mrefu hapa, na anaendelea vizuri sana na anafunga mabao mengi.”
Guardiola alikiri kwamba timu yoyote ingependa kuwa na mshambuliaji huyo pia, rais wa Barca, Laporta anamheshimu sana Haaland.
“Unaweza kuniambia klabu moja ambayo haitamani kuwa na Erling Haaland?” Ninaelewa Barcelona inamtaka Erling, na pia klabu zote duniani zinamtaka, vilevile sisi pia kama asingekuwa kwetu ingekuwa ni ndoto yetu kuwa naye.”
Taarifa za hivi karibuni zilifichua kwamba Haaland amechoshwa na kiwango cha Man City, hivyo anahitaji kuondoka ili kutua timu ambayo itampa nafasi ya kufanya vizuri zaidi kwa kushinda mataji makubwa na mwishowe aweze kuwania tuzo kubwa kama ilivyokuwa kwa wenzake waliopo, Real Madrid, Barca, PSG kwani anaamini alipaswa kuwa miongoni mwa wachezaji watatu wa juu waliokuwa wanawania tuzo ya Ballon D’or mwaka huu.