Pyramids, Stade Malien zashinda zikienda robo fainali, Lupopo yaitibulia Mamelodi
Muktasari:
- Mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Pyramids imejikita kileleni mwa Kundi A la baada ya kuonyesha ubabe kipindi cha pili na kuibuka na ushindi wa mabao 4–1 dhidi ya Rivers United ya Nigeria jana Jumapili.
STADE Malien imeifunga Esperance na kujihakikishia nafasi ya kucheza robo fainali huku Pyramids ikitinga hatua hiyo kwa kishindo ikiichapa River United ya Nigeria kwa mabao 4-1.
Mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Pyramids imejikita kileleni mwa Kundi A la baada ya kuonyesha ubabe kipindi cha pili na kuibuka na ushindi wa mabao 4–1 dhidi ya Rivers United ya Nigeria jana Jumapili.
Timu hiyo ya Misri iligeuza matokeo baada ya kuwa nyuma kipindi cha kwanza kwenye Uwanja wa Godswill Akpabio mjini Uyo na kujihakikishia kufuzu robo fainali, huku ikisaliwa na mechi moja mkinoni.
Rivers United iliwashtua wageni wao dakika ya 33, baada ya Stephen Manu kupiga shuti kali la mbali lililomshinda kipa na kuwapa wenyeji uongozi.
Hata hivyo, huo ulikuwa mwanzo na mwisho wa upinzani wao.
Kipindi cha pili, Pyramids ilirudi kwa nguvu mpya na kuanza kutawala mchezo. Dakika ya 53, Mostafa Fathi alipokea pasi safi kutoka kwa Mostafa Zico na kufunga bao la kusawazisha.
Bao hilo lilibadilisha kabisa mwelekeo wa mchezo.
Rivers United ilijikuta ikirudi nyuma huku Pyramids ikitawala na kulazimisha makosa kadhaa ya safu ya mabeki ya wenyeji.
Dakika ya 77, Pyramids ilipata penalti baada ya mpira kugusa mkono ndani ya eneo la hatari. Marwan Hamdi alifunga kwa utulivu na kuiweka timu yake mbele.
Rivers ilipojaribu kusaka sare, ilifunguka zaidi na kuacha mianya.
Mchezaji wa akiba Awda Al-Fakhoury alifunga bao lake la kwanza kwa klabu dakika ya 88, kabla ya Nasser Maher kuongeza la nne dakika za nyongeza na kukamilisha ushindi mkubwa ndani ya dakika 14 za mwisho.
Matokeo hayo yanaifanya Pyramids kufikisha pointi 13 kileleni mwa Kundi A na kufuzu rasmi hatua ya mtoano.
Rivers United imesalia mkiani na pointi moja tu na imeondolewa rasmi mashindanoni.
Stade Malien 1–0 Esperance
Timu ya Stade Malien ilijihakikishia nafasi ya kucheza robo fainali baada ya ushindi mwembamba wa 1-0 dhidi ya Esperance de Tunis katika mechi kali ya Kundi D.
Mchezo huo ulikuwa wa tahadhari kubwa, huku timu zote zikilinda zaidi kuliko kushambulia kipindi cha kwanza.
Esperance ilitawala umiliki wa mpira, lakini ilishindwa kupenya safu ya ulinzi wa Mali iliyokuwa imara.
Dakika ya 54, Stade Malien ilipata bao la pekee na la ushindi kupitia kwa Koro Kouyali, baada ya shambulizi lililopangwa vizuri kuwavuruga wapinzani kwa muda mfupi.
Esperance iliongeza mashambulizi ikisaka nafasi ya kusawazisha, lakini mabeki wa Stade Malien walikuwa thabiti hadi mwisho wa mchezo.
Ushindi huo unaiweka Stade Malien kileleni mwa Kundi D na kuihakikishia kufuzu robo fainali mapema. Esperance ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi sita, na italazimika kupata matokeo mazuri katika mechi ya mwisho ili kujihakikishia nafasi ya kusonga mbele.
FC Lupopo 1–1 Mamelodi Sundowns
Matumaini ya Mamelodi Sundowns kufuzu mapema kutoka Kundi C yalipata pigo jingine baada ya kulazimishwa sare ya 1–1 mbele ya Saint Éloi Lupopo ya DR Congo.
Sundowns ilipoteza pointi kwa mara ya pili mfululizo, hali inayofanya kundi hilo kubaki wazi huku mechi ya mwisho ikisubiriwa kwa presha kubwa.
Sundowns ilianza vizuri na karibu ifunge ndani ya dakika ya kwanza kupitia kwa Khulumani Ndamane, lakini kichwa chake kilipita karibu na lango.
Dakika ya 10, Lupopo ilitumia vizuri nafasi baada ya kuuvunja mtego wa kuotea na kumruhusu Enock Moila kufunga kwa karibu na kuipa timu yake uongozi.
Sundowns ilitawala umiliki wa mpira lakini ilishindwa kupenya safu ya ulinzi wa Lupopo.
Kipindi cha pili, dakika ya 54, Jayden Adams alisawazisha kwa kichwa kizuri kilichoingia kona ya juu ya lango.
Sundowns iliendelea kushambulia wakisaka ushindi, lakini ilikosa bahati baada ya Teboho Mokoena kupiga mpira uliogonga mwamba wa lango dakika za mwishoni.
Sare hiyo inaacha Sundowns ikiwa na kazi kubwa katika mechi ya mwisho ya makundi, huku Lupopo ikiendelea kuwa na matumaini ya kufuzu.