Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yanga, Azam hesabu ngumu robo fainali CAF

HESABU Pict


UKWELI ndivyo ulivyo. Simba imeshatoka kabisa kwenye ndoto za kwenda robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Hii ni baada ya wikiendi kutoka sare ya 1-1 na Petro Atletico ya Angola. Hesabu zimebaki kwa Yanga iliyopoteza ugenini kwa bao 1-0 mbele ya AS FAR Rabat ya Morocco katika Ligi ya Mabingwa Afrika na Azam FC iliyopo Kombe la Shirikisho Afrika baafa ya kushinda mechi ya tatu mfululizo ya Kundi B.


Timu hizo mbili zinasubiri mechi za mwisho wikiendi hii kuamua hatia yao, huku kimahesabu ikionekana kuwa nguvu kwani zinahitajika hesabu za vidole na kuombea wapinzani wengine wa makundi yao kupata matokeo mabaya ili zenyewe zipenye.


Hesabu hizo ngumu za kwenda robo fainali zipo pia kwa Singida Black Stars iliyopo Kombe la Shirikisho Afrika ambayo usiku wa jana ilikuwa uwanjani kumalizana na CR Belouizdad kabla ya kuifuata Stellenbosch ya Afrika Kusini ugenini kuona kama itafanya maajabu ya kuvuka hapo ilipo.

Ukiachana na Simba iliyokwama mapema kuvuka hatua hiyo kwenda robo fainali kwa mara ya kwanza tangu ilipoanza kutinga makundi ya michuano ya CAF kuanzia msimu wa 2018-2019, huku Singida yenyewe ilikuwa inategemea matokeo ya jana kujua inajiweka wapi, lakini kwa Yanga na Azam zina dakika 90 kila moja kuamua hatma yao, ikipiga hesabu kila moja ni lazima ishinde huku zikiombea mabaya wapinzani wao wanaochuana nao kundini.

Mwanaspoti linakuchambulia mechi zilizopigwa mwishoni mwa wiki iliyopita kwa wawakilishi hao wa Tanzania na namna hesabu zilivyo ngumu ni miujiza pekee inayoweza kuzivusha kwenda robo fainali, la sivyo mambo yatakuwa wameisha hapo kwa timu zote nne kuaga michuano hiyo ya Afrika.


HESABU ZA SIMBA

Simba ilimaliza safari yake rasmi wiki iliyopita ikiwa nyumbani baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 na Esperance ya Tunisia, kisha kujitibulia zaidi kwa kutoka sare nyingine ya 1-1 ugenini dhidi ya juzi dhidi ya Petro Atletico ya Angola tena ikicheza pungufu kwa zaidi ya dakika 50 za mechi hiyo ya Kundi D baada ya beki wa kulia na nahodha wa timu hiyo, Shomari Kapombe kupewa kadi mbili za njano mbili zilizozaa nyekundu ndani ya dakika 40 za kwanza.

ZENG 05

Kama isingekuwa kadi ile basi pengine Simba ingefanya vizuri zaidi, kwani licha ya kutangulia kuruhusu bao mapema dakika ya 13, kisha baadaye kucheza pungufu, Wekundu hao walitulia na kuwabana vizuri Petro huku wakicheza soka la mashambulizi ya kushtukiza.

Simba inaendelea kuimarika ambapo ukitazama namna bao lake la kusawazisha wakitumia akili ya kupokonya mpira wakitumia pasi tatu tu kutoka kwa winga Inno Loemba kisha kumpa Anicet Oura ambaye kabla ya kwenda kufunga alimuona Seleman Mwalimu pembeni kisha kwenda kusuburia mpira kati na kumalizia kwa akili kubwa.

Simba ilichelewa kuwaka kwenye mashindano haya kutokana na mabadiliko ya kikosi na hata benchi la ufundi lakini kwa namna ilivyocheza mechi hizi mbili za mwisho kabla ya mchezo wa kufungia makundi wekundu hao wanaonekasna kuimarika taratibu.

ZENG 03

Simba imefikisha pointi mbili ambapo juzi ilipata pointi ya kwanza ugenini katika mechi zake tatu na sasa itaisubiria nyumbani Stade Malien ya Mali katika mechi ya mwisho itakayopigwa wikiendi hii ili kukamilisha ratiba kwani haitakuwa na safari yoyote hata ikishinda kwa mabao mengi hii ni kwa sababu hadi sasa timu hiyo imekusanya pointi mbili tu kupitia mechi tano na ikishinda itafikisha tano ambazo zimeshapitwa na wapinzani wengine wa kundi hilo ikiwamo Petro iliyopo nafasi ya tatu katika kundi hilo itakayomalizana na Esperance.

Hii ni rekodi mbaya kwa Simba katika michuano ya CAF ikitinga makundi tangu 2018-2019 na sasa kilichobaki ni kutafuta ushindi wa kwanza Afrika kwa msimu huu ikiwa nyumbani, kwani katika mechi nne zikiwamo mbili za raundi ya awali na nyingine mbili za makundi imeishia kutoka sare na kupoteza tu.

ZENG 01

Simba ilianza kwa kutoka sare ya 1-1 na Gaborone United ya Botswana katika raundi ya kwanza kisha kutoka suluhu na Nsingizini Hotspurs ya eSwatini kabla ya kufungwa 1-0 na Petro hatua ya makundi na kutoka sare ya 2-2 na Esperance wiki iliyopita na sasa inajiandaa kuipokea Malien.

Simba iliyofika fainali ya Kombe la Shirikisho msimu uliopita na kupoteza kwa jumla ya mabao 3-1 mbele ya RS Berkane ya Morocco ni mwaka 2002 tu ndipo iliishinda makundi, lakini mara nyingine zote ilikuwa ikikwamia robo fainali ya Ligi ya Mabingwa na Shirikisho Afrika.


AZAM FC HUKO NAKO

Azam imeweka rekodi bora ya kushiriki hatua ya makundi ya michuano ya CAF kwa mara ya kwanza, ikiwa Kombe la Shirikisho Afrika kwa kuvuna pointi nyingi ambazo hazijawahi kufikiwa na klabu yoyote tangu Uhuru wa Tanganyika kwa ushiriki wa mara ya kwanza wa hatua hiyo ya makundi.

HESA 03

Azam iipata ushindi wa tatu mfululizo baada ya kuichapa AS Maniema ya DR Congo kwa bao 1-0 kwenye uwanja wa nyumbani wa New Amaan Complex, Unguja na kufikisha pointi tisa ambazo hakuna timu ambayo kutoka Tanzania imewahi kufikisha iliposhiriki mechi za hatua hii kwa mara ya kwanza.

Ushindi huo wa Azam kwa bao la kichwa la kiungo mkabaji, Sadio Kanoute limelifanya kundi lake kuwa gumu likisubiri mechi za mwisho kuamua nani anakwenda robo fainali ambapo matajiri hao watakuwa wanawania nafasi hizo dhidi ya Wydad Athletic iliyokuwa uwanjani ugenini jana dhidi ya Nairobi United na Maniema ambao wanalingana nao pointi.

Ugumu ni kwamba Azam inatakiwa kusafiri kuifuata Wydad katika mechi ya mwisho ikihitaji ushindi kama ambavyo waarabu hao lakini Maniema nao wakiwa nyumbani itamalizana na vibonde Nairobi Utd ambapo matokeo yoyote ya ushindi yataibeba Wakongomani kutokana na matokeo ya jumla baina yao na Azam kama Wanalambalamba watafanya maajabu ya kuifunga Wydad ikiwa kwao Morocco.

HESA 02

Kama Azam itapoteza mchezo wa mwisho itairahisishia kazi Maniema ambao hata kama watapata sare au ushindi, matajiri hao wa Chamazi wataishia hapo na kuziacha Wydad na Maniema zikienda robo fainali. Lakini kama Maniema itashinda na Azam itashinda kila moja itafikisha pointi 12 na Wakongoman wataenda robo na Wydad kwa sababu katika mechi baina ya timu hizo mbili, Maniema ilishinda nyumbani 2-0 na kupoteza ugenini kwa bao 1-0.

Hapo ndipo hesabu zinapoonekana kuwa ngumu kwa Azam, ingawa yenyewe haina cha kupoteza kwani hata kuvuna pointi tisa kwao imekuwa kama maajabu kwa sababu kundi lilionekana kuwa gumu, lakini kocha Florebnt Ibenge na wachezaji walipambana na kukusdanya pointi hizo tisa.

Kwa wanaokumbuka Yanga ikicheza makundi kwa mara ya kwanza mwaka 1998 katika Ligi ya Mabingwa ilimaliza na pointi nne, ilihali Simba ikicheza makundi kwa mara ya kwanza 2003 katika Ligi ya Mabingwa Afrika kama ilivyokuwa Yanga, ilivuna pointi saba, wakati Yanga ikirudi Kombe la Shirikisho Afrika ikiwa klabu ya kwanza kufanya hivyo ilivyofanya katika Ligi ya Mabingwa ilipokuwa pia ya kwanza ilivuna pointi nne tu.

Namungo, timu nyingine iliyocheza makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika 2020-2021 iliweka rekodi ya kipekee ya kutoshinda wala kufunga bao au kuvuna pointi yoyote kupitia mechi sita ilizocheza katika kundi lililokuwa na Nkana ya Zambia, Raja Casablanca ya Morocco na Pyramids ya Misri. Kama Azam ikienda robo fainali itakuwa imepiga hatua kubwa, lakini hata kama ikikwama ina kitu kikubwa cha kujivunia ambapo ni Singida Black Stars pekee ambayo kama ikishinda mechi zake mbili ule wa jana na ule wa mwisho itaweza kufikisha pointi walizonazo ikiwa Kundi C lenye klabu za Stellenbosch ya Afrika Kusini, CR Belouizdad ya Algeria na Otoho d’Oyo ya Congo Brazzaville.

HESA 01

Azam inatakiwa kwenda na hatua kubwa nchini Morocco kwenda kulipiza kisasi ikitaka kuweka historia mpya ingawa haitakuwa rahisi kwao kwani Waarabu hao wameshinda mechi zake mbili za ugenini kwenye kundi lao na anayekwenda kumalizia mchezo wa tatu ni wao.


UGUMU KWA YANGA

Yanga nao ni kama imeahirisha kesi ikijiweka eneo gumu baada ya kupoteza ugenini kwa bao 1-0 mbele ya AS FAR Rabat ya Morocco na sasa matumaini pekee ya mabingwa hao wa Tanzania ni kushinda mechi ya mwisho nyumbani, huku ikiomba dua mbaya kwa Wamorocco hao wapoteze mchezo wa mwisho ugenini dhidi ya Al Ahly ya Misri.

ZENG 02

Yanga tiketi ilikuwa kwao kama ingeshinda jana, lakini ikashindwa kufanya hivyo ambapo hata nafasi zile bora ilikuja kuzitengerneza kipindi cha pili ikipoteza nafasi tatu za wazi ambazo zingeweza kuwapa tiketi ya kwenda robo.

Yanga ilicheza vizuri mechi hiyo ya juzi hasa kwenye ukuta wake, mabeki wake walifanya kazi kubwa wakiongozwa na nahodha wao Bakari Mwamnyeto na wenzake lakini kosa moja la kumsahau beki wa kulia wa FAR Rabat, Anas Bach likaharibu hesabu zao.

Yanga ingeweza kuruhusu bao hilo mapema kama FAR Rabat wangekuwa makini, kwani Bach katika dakika ya 55 alikaribia kufunga kama ambavyo alifanya kwa kutumia madhaifu ya wapinzani wake ambapo kiungo wa pembeni wa wageni alikuwa anashindwa kurudi chini kuja kuwasaidia mabeki wa kushoto.

ZENG 03 (1)

Ukweli ni kwamba kocha Pedro Goncalves atajilaumu kwa kuchelewa kumtoa Pacome Zouzoua ambaye alikuwa amechoka na akikosea hesabu zake nyingi kwenye kujenga mashambulizi ya Yang, akiwa pia harudi chini kwa wakati kuwasaidia wenzake.

Yanga sasa inatakiwa kuhakikisha inashinda vizuri nyumbani tena kwa ushindi zaidi ya mabao 2-0, huku wakiiombea dua mbaya FAR Rabat ipoteze ugenini mbele ya Ahly pia kwa kipigo si chini ya 2-0 ili tiketi yao iwe hai kwenda robo, kwani kwa sasa Al Ahly inaongoza kundi ikiwa na pointi tisa, ikifuatiwa na wamorocco wenye nane na Yanga ikisaliwa na tano.

Kama Yanga itashinda mbele ya JS Kabylie yenye pointi tatu, itafikisha pointi nane, lakini uwiano wa mabao unaweza kuiangusha kama Al Ahly itashinda kwa bao 1-0 dhidi ya FAR Rabat kwa vile matokeo ya jumla baina yao (head to head) zimetoshana nguvu kwa sare ya 1-1, kila moja ikishinda nyumbani kwa bao 1-0.

ZENG 06

Hapo ndipo unapoona hesabu za Yanga zinakuwa ngumu zaidi, kwani matokeo ya sare yoyote baina ya Al Ahly na FAR Rabat au yenyewe kupata ushindi kiduchu utaing’oa na kushindwa kufuzu robo fainali kwa msimu wa pili mfululizo kwani msimu uliopita ilikwamba mbele ya MC Alger ya Algeria.