PSG kutangaza ubingwa leo?

Muktasari:

  • PSG leo itakuwa pale kwenye dimba lao la nyumbani Parc des Princes  kuvaana na Le Havre na kama itashinda itatwaa ubingwa wa Ligi Kuu Ufaransa kwa msimu huu.

PARIS, UFARANSA: Baada ya safari ya muda mrefu tangu mwaka jana, hatimaye siku iliyokuwa inasubiriwa kwa hamu na mashabiki wa Paris Saint-Germain imewadia.

PSG leo itakuwa pale kwenye dimba lao la nyumbani Parc des Princes  kuvaana na Le Havre na kama itashinda itatwaa ubingwa wa Ligi Kuu Ufaransa kwa msimu huu.

Hadi sasa matajiri hao wa Jiji la Paris wana alama 69 na wamecheza mechi 30 za michuano yote, sawa na mpinzani wake wa karibu AS Monaco iliyocheza mechi 30 na kukusanya pointi 58.

Kiujumla mechi zilizobakia ni nne tu na kama Monaco itashinda zote itakuwa imekusanya alama 70, wakati PSG kama itashinda leo itaifikisha pointi 72 ambazo hazitafikiwa na timu nyingine yoyote.

Uwezekano wa PSG kushinda mechi hii unaonekana kuwa mkubwa zaidi kwa sababu ya kiwango ambacho Le Havre imekionyesha msimu huu ambapo hadi sasa ipo kwenye nafasi mbaya za kucheza mtoano kwa ajili ya kubaki Ligue 1.

Mbali ya fomu yao ya sasa, historia inaonyesha kwamba tangu timu hizi zianze kukutana Le Havre haijawahi kushinda hata mara moja dhidi ya PSG ikipoteza mechi zote nane walizokutana.

Mechi ya mwisho wakiwa nyumbani Le Havre ilikubali kichapo cha mabao 2-0.

Huu utakuwa ni ubingwa wao wa 12 ndani ya Ligue 1 na pia itakuwa inauchukua kwa mara ya tatu mfululizo kuanzia msimu wa 2021/22 na 2022/23.

Wakati PSG ina kazi ya kujihakikishia ubingwa leo, pia kutakuwa na mechi nyingine ambazo zinakutanisha timu zinazopambana kufuzu Ligi ya Mabingwa na wengine kusalia katika ligi.

Hadi sasa Ufaransa ina nafasi nne za kupeleka timu katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na PSG imeshajihakikishia nafasi hiyo kutokana na alama zake.

Lakini timu itakayoshika nafasi ya nne lazima itacheza hatua za awali kabla ya kufuzu kucheza hatua ya makundi ambapo timu tatu za juu zitafuzu moja kwa moja.

Kutokana na msimamo ulivyo, Monaco na Brest ndio zipo kwenye nafasi ya kufuzu hatua ya makundi ya igi ya Mabingwa moja kwa moja huku Lille iliyopo nafasi ya nne iko katika ukanda wa kuanzia katika hatua za awali.

Lakini lolote linaweza kutokea kwani jumla ya mechi zilizobakia kabla ya ligi kuisha ni nne.

Utofauti wa alama baina ya Lille na timu hizi zinazoshika nafasi ya pili na tatu kwenye msimamo wa Ligue 1 ni pointi moja kwa Brest pia ni pointi sita kwa Monaco iliyopo nafasi ya pili.