PSG ilivyoitupa nje Arsenal, yatinga fainali Ligi ya Mabingwa Ulaya

Muktasari:
- Mabao ya ushindi kwa PSG yamefungwa na kiungo, Fabián Ruiz katika dakika ya 27 na beki wa kulia Achraf Hakimi dakika ya 72, huku bao pekee la Arsenal likifungwa na Bukayo Saka dakika ya 76.
PARIS, UFARANSA: PSG imefanikiwa kufuzu katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kuifunga Arsenal mabao 2-1 katika mchezo wa marudiano wa nusu fainali uliochezwa kwenye Uwanja wa Parc des Princes.

Kwa ushindi huo, PSG imetinga katika fainali kwa jumla ya ushindi wa mabao 3-1 baada ya sare ya 1-1 katika mchezo wa kwanza uliofanyika kwenye Uwanja wa Emirates.
Ushindi huo umeipeleka PSG katika fainali ya pili ndani ya miaka mitano, na sasa itakabiliana na Inter Milan ambayo iliiondoa Barcelona kwa jumla ya mabao 7-6. Fainali hiyo inatarajiwa kuchezwa Mei 31, 2025 kwenye Uwanja wa Allianz Arena, jijini Munich, Ujerumani.

Arsenal ilianza kwa kasi, ikitawala mchezo katika dakika za mwanzo na kujaribu kuishambulia PSG. Hata hivyo, PSG walijibu mapigo na kufanikiwa kupata bao la kwanza kupitia kwa kiungo, Fabián Ruiz katika dakika ya 27. Bao hilo liliwapa PSG uongozi mpaka kipindi cha kwanza kinamalizika.

Katika kipindi cha pili, PSG waliendelea kuonyesha ubora na kuongeza bao la pili kupitia kwa beki, Achraf Hakimi katika dakika ya 72. Arsenal walijitahidi kurudi mchezoni na kufanikiwa kupata bao la kufutia machozi ambalo lilifungwa na Bukayo Saka katika dakika ya 76. Hata hivyo, juhudi zao hazikutosha kuzuia PSG kusonga mbele.

Ni timu mbili pekee ndizo zilizowahi kufuzu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kupoteza mchezo wa kwanza wa nusu fainali wakiwa nyumbani ambapo Ajax waliwahi kufanya hivyo dhidi ya Panathinaikos msimu wa mwaka 1995-96, na Tottenham dhidi ya Ajax msimu wa mwaka 2018-19.
Mchezo wa kwanza Ajax walifungwa nyumbani bao 1–0 na Panathinaikos katika mchezo wa marudiano Ajax walishinda 3–0 ugenini, ambapo walishinda jumla ya mabao 3–1 na kufuzu fainali.

Tottenham Hotspur katika msimu wa 2018–19 walipoteza katika mchezo wa kwanza wa nyumbani wakifungwa 1–0 na Ajax. Mchezo wa marudiano uliochezwa jijini Amsterdam, Tottenham walifuzu katika fainali kwa bao la ugenini licha ya sare ya jumla ya mabao 3–3, na walicheza fainali dhidi ya Liverpool.

Kwa upande wa Arsenal, ndoto ya kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya imefikia kikomo msimu huu. Licha ya kuonyesha mchezo mzuri na juhudi, wameshindwa kuikabili PSG na hatimaye kuondolewa katika hatua ya nusu fainali.