Premier League yajishtukia, yafuta ujumbe wa kuikebehi Spurs
Muktasari:
- Hadi kufikia leo Jumatatu asubuhi, Ligi Kuu ilikuwa imeshafuta ujumbe huo, ingawa tayari ulikuwa limeshaonekana na mamia ya maelfu ya watu duniani kote.
UONGOZI wa Ligi Kuu ya England, umelazimika kufuta ujumbe katika mitandao ya kijamii ulioonekana kuifanyia dhihaka klabu ya Tottenham Hotspur baada ya kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya Fulham, jana Jumapili, Machi Mosi, 2026.
Kupitia ukurasa wake wa X (zamani Twitter), Ligi Kuu England maarufu Premier, ilipakia video ikimwonyesha kipa wa Spurs, Guglielmo Vicario, akipiga mpira wa adhabu uliotoka nje moja kwa moja, huku ujumbe huo ukiambatana na maneno ya kejeli: "Ndivyo mpango ulivyochorwa" na "Shuti la kuvutia kutoka kwa Vicario," ukiwa na emoji za kucheka hadi kulia.
Ujumbe huo ulizua mjadala mkali, huku watumiaji wengi wa mitandao wakikosoa kitendo cha ligi hiyo kuifanyia mzaha klabu mwanachama, jambo ambalo lilionekana kutokuwa la kitaalamu.
Gazeti la Daily Mail Sport limeripoti kuwa viongozi wa Tottenham, ambao kwa sasa wanapambana kukwepa kushuka daraja, walistushwa na chapisho hilo na kuwasilisha malalamiko yao rasmi kwa mabosi wa Ligi Kuu. Ingawa Spurs inakubali imekuwa na msimu mbaya, iliamini haikupaswa kufanyiwa ‘utani’ huo na chombo kinachosimamia mashindano hayo.
Hali hiyo imekuja wakati mbaya kwa Spurs, kwani kipigo hicho dhidi ya Fulham ni cha nne mfululizo, jambo linawafanya kuwa na pointi nne pekee juu ya mstari wa kushuka daraja.
Kocha mkuu wa Spurs, Igor Tudor, ambaye alichukua mikoba ya Thomas Frank mwezi uliopita, alionekana kukasirishwa na matokeo hayo huku akimshambulia mshambuliaji wa Fulham, Raul Jimenez, akimwita ‘mdanganyifu'.
"Ni hali ngumu na yenye matatizo mengi," amesema Tudor kwa hasira baada ya kikosi chake kufikisha mechi 10 bila ushindi.
"Tunahitaji kupata sauti ndani yetu. Tunahitaji mchezaji mwenye hulka na utayari wa kupambana."
Tudor alikiri kuwa Fulham walikuwa bora zaidi uwanjani, wakikimbia zaidi na kufanya uamuzi wa haraka kuliko wachezaji wake ambao walionekana kuchelewa katika kila hatua.
Hadi kufikia leo Jumatatu asubuhi, Ligi Kuu ilikuwa imeshafuta ujumbe huo, ingawa tayari ulikuwa limeshaonekana na mamia ya maelfu ya watu duniani kote.