Rodrygo Liverpool, Dominic Szoboszlai Real Madrid
Muktasari:
- Madrid imekuwa ikihitaji huduma ya Dominic wa muda mrefu lakini haionekani kama watakuwa tayari kufanya mabadilishano ya wachezaji.
LIVERPOOL inafikiria kufanya mabadilishano ya wachezaji na Real Madrid na itamchukua winga wa kimataifa wa Brazil, Rodrygo, 25, kutoka timu hiyo kisha wao kumwachia kiungo wao wa kimataifa wa Hungury, Dominik Szoboszlai, 25, kwenda kwa vigogo hao wa Hispania.
Madrid imekuwa ikihitaji huduma ya Dominic wa muda mrefu lakini haionekani kama watakuwa tayari kufanya mabadilishano ya wachezaji.
Rodrygo alihusishwa sana kuondoka dirisha lililopita la majira ya kiangazi. Mkataba wake wa sasa unamalizika mwaka 2027.
Taarifa zinaeleza kwa sasa mazungumzo yanaendelea na timu hizo zinaweza kufikia mwafaka baada ya msimu kumalizika.
Awali Madrid iliripotiwa kuwa tayari kumwachia Rodrygo kwa ofa itakayofikia Pauni 70 milioni lakini baadae taarifa zikaeleza imesitisha kumuuza kwani bado ina mipango naye.
Tangu kuanza kwa msimu huu Rodrygo amecheza mechi 26 za michuano yote, amefunga mabao matatu na kutoa asisti sita.
Scott McTominay
MANCHESTER United inaangalia uwezekano wa kumsajili kiungo wa Napoli, Scott McTominay katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Taarifa zinadai mabosi wa Man United, wapo tayari kutoa Pauni 70 milioni kuhakikisha inamrudisha mchezaji wao huyo wa zamani. Napoli inaonekana kuwa tayari kumuuza kiungo huyu mwenye umri wa miaka 29, ambaye ni miongoni mwa wachezaji tegemeo wa kikosi chao.
Micky van de Ven
REAL Madrid inamfuatilia kwa karibu beki wa kati wa Tottenham Hotspurs, Micky van de Ven, mwenye umri wa miaka 24. Hata hivyo, inaelezwa staa huyo wa kimataifa wa Uholanzi yupo katika mazungumzo ya kusaini mkataba mpya wa kuendelea kusalia katika viunga vya Spurs. Madrid imekuwa ikimtazama kwa muda mrefu na inaonekana kuridhishwa na kiwango chake aliocho onyesha tangu msimu uliopita.
Ibrahim Sangare
MANCHESTER United imevutiwa sana na kiungo wa Nottingham Forest, Ibrahim Sangare, 28, ambaye inataka kumfanya kuwa mbadala wa kiungo wao wa kimataifa wa Brazil, Casemiro, 34, anayetarajiwa kuondoka mwisho wa msimu huu. Sangare anaonekana kufanana kiuchezaji sawa na Casemiro pia umri wake unaonekana kuwa sahihi kwa sababu tayari ameshacheza kwa muda mrefu hivyo ana uzoefu.
Antoine Griezmann
MSHAMBULIAJI wa Atletico Madrid na timu ya taifa ya Ufaransa, Antoine Griezmann mwenye umri wa miaka, 34, yupo katika mazungumzo na Orlando City ya Marekani ambayo anatarajiwa kujiunga nayo katika dirisha ljalo la majira ya kiangazi. Kwa muda mrefu, Griezmann amekuwa akihusishwa na mpango wa kutaka kucheza Ligi Kuu Marekani baada ya kuondoka Atletico.
Liam Delap
KOCHA wa Chelsea, Liam Rosenior inadaiwa kutokuwa na mpango wa kumruhusu straika wa timu hiyo Liam Delap kuondoka dirisha lijalo la majira ya kiangazi kwa sababu anaamini anaweza kuwa mchezaji tegemeo na akaipa faida timu. Delap, 23, hivi karibu alihusishwa na kuondoka mwisho wa msimu na Everton inataji kumsajili. Staa huyu kwa sasa hapati nafasi ya kutosha kikosi cha kwanza hali inayosababisha kuibuka kwa tetesi hizi.
Andy Robertson
ASTON Villa, Crystal Palace na Wolves ziko vitani kuiwania saini ya beki wa kushoto wa Liverpool na timu ya taifa ya Scotland, Andy Robertson, ambaye ana umri wa miaka 31. Robertson ambaye kwa sasa anapata nafasi kubwa ya kucheza kikosi cha kwanza cha Liverpool baada ya majeruhi kuzidi kuongezeka, awali hakuwa akipata nafasi ya mara kwa mara hali iliyosababisha afikirie kuondoka.
Igor Jesus
NOTTINGHAM Forest ipo tayari kusikiliza ofa kutoka timu zitakazohitaji huduma ya staa wao, Igor Jesus, 24, ifikapo mwisho wa msimu huu. Inadaiwa licha ya Forest kutoonyesha kiwango bora kwa msimu huu, timu nyingi zimevutiwa sana na Igor ambaye ameendelea kuwa bora mbali ya changamoto za timu. Mabosi wa Forest wanahitaji kiasi kisichopungua Pauni 60 milioni ili kumuuza fundi huyu.