Polisi wajitetea mashabiki Maccabi Tel Aviv kuzuiwa England
Muktasari:
- Serikali imesema iko tayari kugharamia ulinzi wowote utakaohitajika ili kuruhusu mashabiki wa Maccabi kuhudhuria, lakini klabu hiyo ya Israeli ilikataa mgao wao wa tiketi.
BIRMINGHAM, ENGLAND: Kamishna Mkuu wa Polisi wa West Midlands, amesema jeshi hilo halijashindwa kumlinda mtu yeyote akitetea uamuzi wa kuwapiga marufuku mashabiki wa Maccabi Tel Aviv kuhudhuria mechi ya Europa League dhidi ya Aston Villa, mwezi ujao.
Tangazo la Birmingham Safety Advisory Group (SAG) kuzuia mashabiki wa timu hiyo ya Israeli kusafiri kuhudhuria mechi hiyo itakayochezwa Novemba 6, 2025 kwa sababu za kiusalama, limekosolewa vikali na wanasiasa, wakiwemo waziri mkuu wa Uingereza.
Serikali imesema iko tayari kugharamia ulinzi wowote utakaohitajika ili kuruhusu mashabiki wa Maccabi kuhudhuria, lakini klabu hiyo ya Israeli ilikataa mgao wao wa tiketi.
Hata hivyo, Kamishna Mkuu, Craig Guildford amesema Jumatano kuwa anaheshimu uamuzi huo ambao ulitolewa kwa kuzingatia taarifa za kiintelijensia, akisisitiza: “Birmingham haijashindwa kumlinda mtu yeyote, wala Polisi wa West Midlands hawajashindwa.”
Kikundi cha ushauri wa usalama cha Birmingham (SAG), ambacho ndicho chenye mamlaka ya kutoa vyeti vya usalama kwa mechi na kinaundwa na polisi, Halmashauri ya Jiji la Birmingham, pamoja na idara za zimamoto na huduma za dharura, kilimjulisha Aston Villa wiki iliyopita kwamba mashabiki wa timu ya ugenini hawangeruhusiwa.
Guildford amesema kwamba licha ya msaada mzuri kutoka serikalini, maafisa wake walizingatia hatari hizo kitaalamu na kutoa ushauri ipasavyo.
“Nimesoma baadhi ya taarifa za kijasusi na tathmini zilizotolewa. Zimefanywa kwa uamuzi wa kitaalamu,” amesema.
Tathmini za hatari zilizopelekea marufuku hiyo hazijachapishwa hadharani, lakini gazeti The Guardian limedai polisi walihitimisha kuwa hatari kubwa ya vurugu ilitokana na mashabiki wenye misimamo mikali wa klabu ya Israeli.
Guildford ameongeza kuwa jeshi lake litaendelea kutoa ushauri kwa SAG na kuheshimu uamuzi wa kikundi hicho.
“Uamuzi ukishafanywa, ni lazima uheshimiwe. Yanazingatia uelewa mzuri wa tishio na hatari. Kazi yetu kama polisi ni kuhakikisha kila mtu anakuwa salama,” amesema.
Kiongozi huyo amekataa madai kwamba imani ya jamii kwa polisi imepungua kufuatia marufuku hiyo.
“Tunajitahidi kwa uwezo wetu wote, kuanzia mimi hadi maafisa wa chini, kuhakikisha jamii ina imani nasi.
“Tunapokea maoni mengi chanya kuhusu jinsi tunavyowahakikishia usalama. Hatuwezi, na hatutawahi, kumridhisha kila mtu,” amesema.
Jumapili iliyopita, mechi ya Ligi Kuu ya Israel kati ya Maccabi Tel Aviv na Hapoel Tel Aviv iliahirishwa kabla haijaanza kufuatia kile polisi walichokiita vurugu na machafuko ya umma.
Aston Villa sasa imetangaza sera yao ya utoaji tiketi kwa mechi hiyo, ikisisitiza kuwa ni mashabiki walio na historia ya kununua tiketi kabla ya msimu huu pekee ndio watakaoruhusiwa kuzipata.
Ubalozi wa Israel nchini Uingereza, umesema unatiwa wasiwasi mkubwa na chuki na uchochezi vilivyosababisha Maccabi kujiondoa kwenye mgao wao wa tiketi.
Katika taarifa yake leo Jumatano Oktoba 22, 2025, Halmashauri ya Jiji la Birmingham imesema: “Kikundi cha Ushauri wa Usalama kiliipatia Klabu ya Aston Villa ushauri kulingana na tathmini ya hatari iliyotolewa na Polisi wa West Midlands.
“Iwapo tathmini ya hatari itabadilika kabla ya mechi, kikundi hicho kitaangalia upya uamuzi wake kama itahitajika.”