Peter Kenyon afichua tatizo lilipo Man United

Muktasari:
- Kenyon, 71, aliyeitumikia Bodi ya Man United kwa miaka sita wakati huo ilipokuwa ikitawala soka la England ndani na nje, alisema anadhani wamiliki hao, familia ya Glazer walifanya kosa kubwa kwa kuruhusu Sir Alex Ferguson na Mkurugenzi Mtendaji Mkuu David Gill kung’atuka klabuni kwa wakati mmoja mwaka 2013 bila ya kuweka mipango thabiti kwa warithi wao.
MANCHESTER, ENGLAND: MKURUGEZNI Mtendaji Mkuu wa zamani wa Mkuu wa Manchester United, Peter Kenyon ametania kwamba familia ya Glazer “Inapaswa kupigwa risasi” kwa kitendo cha kushuhudia timu hiyo ya Old Trafford ikifeli kwa zaidi ya muongo mmoja sasa.
Kenyon, 71, aliyeitumikia Bodi ya Man United kwa miaka sita wakati huo ilipokuwa ikitawala soka la England ndani na nje, alisema anadhani wamiliki hao, familia ya Glazer walifanya kosa kubwa kwa kuruhusu Sir Alex Ferguson na Mkurugenzi Mtendaji Mkuu David Gill kung’atuka klabuni kwa wakati mmoja mwaka 2013 bila ya kuweka mipango thabiti kwa warithi wao.
Kenyon alisema: “Kuporomoka kwa Man United kumetokana na kitendo cha kushindwa kuandaa mpango sahihi kwa warithi. Huwezi kuwaacha watu wawili wenye ushawishi mkubwa katika timu, waliokaa kwa miaka mingi, kocha na mkurugenzi kuondoka kwa wakati mmoja. Hii ni kichekesho. Unapaswa kupigwa risasi kwa jambo hilo.
“Ni biashara gani inaweza kuruhusu waajiriwa wawili wenye nguvu kubwa kuondoka kwa wakati mmoja? Huwezi kujua hata soketi ya umeme ipo wapi! Msinitake niseme mengi. Inanikwaza sana.”
Mashabiki wa Man United wamekuwa wakiandamana mara kadhaa kupiga umiliki wa familia ya Glazer tangu tajiri Malcolm Glazer alipoinunua klabu hiyo mwaka 2005.
Glazer aliacha klabu hiyo katika urithi wa watoto wake watano alipofariki 2014 - na watoto hao wameendelea kuifanya timu kuwa na madeni kwa kutumia kama bondi ya kukopa katika benki mbalimbali huku familia yenyewe ikivuna zaidi ya Pauni 2 bilioni kutoka klabuni hapo.
Familia hiyo ya Kimarekani iliweka kibindoni pia Pauni 1.2 bilioni wakati ilipouza asilimia 27 ya hisa za klabu kwa bilionea Mwingereza, Sir Jim Ratcliffe mwaka jana - lakini klabu bado ina deni la Pauni 1 bilioni linaloiweka katika wakati mgumu wa kuendana na kanuni ya mapato na matumizi endelevu ya EPL na kumnyima kocha mpya, Ruben Amorim fursa ya kuwa na pesa za kusajili.