Pep Guardiola kukaa pembeni Etihad
Muktasari:
- Mhispaniola huyo amekuwa na wakati mzuri kwenye kikosi cha miamba hiyo ya Etihad tangu alipotua mwaka 2016.
MANCHESTER, ENGLAND: KOCHA Pep Guardiola amekiri atang’atuka kwenye kazi yake ya ukocha wakati mkataba wake Manchester City utakapofika tamati.
Mhispaniola huyo amekuwa na wakati mzuri kwenye kikosi cha miamba hiyo ya Etihad tangu alipotua mwaka 2016.
Ameiongoza Man City kubeba mataji sita ya Ligi Kuu England, mawili ya Kombe la FA, manne ya Kombe la Ligi na alisaidia klabu hiyo kubeba taji lao la kwanza la Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Guardiola, 54, mkataba wake utafika tamati 2027 baada ya kusaini dili jipya, Novemba mwaka jana.
Sasa kinachoonekana ni Guardiola tayari ameshaamua kitu atafanya wakati dili hilo litakapofika tamati, atakwenda mapumziko mengine.
Alipoulizwa nini hatima ya maisha yake ya baadaye, alijibu: “Sifahamu.”
“Ukweli, sifahamu, sijui hakika kwa sababu unaweza kuwa na kundi kubwa la watu unaofanya nao kazi wakakuhamasisha tofauti. Ninachojua baada ya kazi hii ya Man City nitasimama, hilo nina hakika, nilishaamua.
“Sifahamu nitasimama muda gani, mwaka mmoja, miwili, mitatu mitano, kumi au kumi na tano, sifahamu. Lakini, nitasimama baada ya kazi hii ya Man City, kwa sababu nataka kuelekeza nguvu kwenye mambo yangu binafsi.”
Guardiola alishawahi kupumzika ukocha kwa mwaka mmoja wakati alipoondoka Barcelona mwaka 2012.
Alirudi kwenye ukocha baada ya kupata dili la kuinoa Bayern Munich mwaka mmoja baadaye.