Ujauzito waiponza Lazio
Muktasari:
- Mahakama ya usuruhushi michezo (CAS) ilitoa uamuzi unaomuunga mkono mchezaji huyo wa Sweden katika kesi ambayo chama cha kimataifa cha wachezaji, FIFPRO, kimeita “kesi ya kihistoria” kuhusu haki za uzazi katika soka.
ROMA, ITALIA: TIMU ya wanawake ya Lazio imeamriwa kulipa fidia kwa kiungo wake wa zamani Maja Gothberg baada ya kubainika kuwa ilisimamisha ajira yake kinyume cha sheria kutokana na ujauzito wake.
Mahakama ya usuruhushi michezo (CAS) ilitoa uamuzi unaomuunga mkono mchezaji huyo wa Sweden katika kesi ambayo chama cha kimataifa cha wachezaji, FIFPRO, kimeita “kesi ya kihistoria” kuhusu haki za uzazi katika soka.
Mbali na fidia, Gothberg pia atalipwa “fidia ya maumivu ya kimaadili” na Lazio.
Mahakama pia ilibaini kuwa Lazio ilifichua taarifa za ujauzito wa Gothberg kwa baadhi ya wachezaji wenzake bila idhini yake, jambo ambalo lilikiuka haki yake ya faragha.
Gothberg alisema “kesi hii haikuhusu soka pekee, bali ilihusu kutendewa kwa haki na heshima katika kipindi muhimu cha maisha yangu.
Uamuzi huu unatuma ujumbe kwamba ujauzito haupaswi kamwe kuonekana kama tatizo au sababu ya kumnyima mchezaji fursa za ajira.”
Jinsi kesi ilivyoanza
Mgogoro huo ulianza mwishoni mwa msimu wa 2023-24, ambapo Gothberg alicheza mechi 29 na kusaidia Lazio kupanda daraja hadi Ligi Kuu ya wanawake nchini Italia.
Alidai kuwa klabu ilikuwa imeanza mazungumzo ya kumpa mkataba mpya na kwamba ingawa mkataba haukusainiwa rasmi, ujumbe wa WhatsApp ulionyesha kuwa masharti muhimu yalikuwa yamekubaliwa.
Kabla ya mkataba huo kukamilishwa rasmi, Gothberg aligundua kuwa alikuwa mjamzito na akaijulisha klabu, licha ya kutokuwa na wajibu wa kisheria kufanya hivyo.
Baada ya taarifa hiyo, Lazio haikutekeleza makubaliano ya awali na baadaye ikadai kuwa Gothberg hakutaka kuendelea kubaki klabuni huku uhusiano kati ya pande hizo ukiharibika.
Kwa mujibu wa sheria za FIFA, klabu lazima ithibitishe kwamba ujauzito haukuwa sababu ya kusitisha ajira ya mchezaji. Aidha, taarifa za ujauzito zinahesabiwa kuwa taarifa za siri za kiafya.
Mkurugenzi wa sheria wa FIFPRO, Alexandra Gomez Bruinewoud, alisema:
“Kesi hii inaonyesha kwamba Kanuni za Uzazi za FIFA si maneno tu yaliyoandikwa kwenye karatasi, bali zinatoa ulinzi wa kweli kwa wachezaji.
Umuhimu wa uamuzi huu unaenda zaidi ya Maja Gothberg na unathibitisha kwamba klabu haziwezi kujiondoa kwenye uhusiano wa ajira mara tu zinapogundua mchezaji ni mjamzito, hata kama mkataba haujakamilishwa rasmi.”
Katika kesi hiyo, Gothberg alipata msaada wa kisheria kutoka FIFPRO na chama cha wachezaji wa Sweden, Spelarforeningen.
Kesi nyingine za kihistoria
Mwaka 2023, nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya wanawake wa Iceland, Sara Bjork Gunnarsdottir, alishinda kesi dhidi ya timu ya wanawake ya Olympique Lyonnais baada ya klabu hiyo kushindwa kumlipa mshahara wake kamili wakati wa ujauzito.
Mahakama ya FIFA iliamuru Lyon kulipa zaidi ya euro 82,000 za mishahara ambayo haikulipwa. FIFPRO ilielezea kesi hiyo kama “alama muhimu ya kihistoria”.
Haki za uzazi katika soka
Mwaka 2024, FIFA ilifanya mabadiliko ya sheria ili kuimarisha ulinzi wa wachezaji na makocha wanawake wakati wa ujauzito, baada ya kujifungua, na hata katika hali za ulezi wa watoto kwa njia ya kuasili.
Miongoni mwa mabadiliko hayo ni:
Moja ni angalau wiki 14 za likizo ya uzazi yenye malipo kamili kwa wachezaji na makocha.
Pili malipo ya asilimia 100 ya mshahara na marupurupu yote kwa kipindi hicho.
Tatu ni haki za likizo kwa wazazi wanaoasili watoto.
Nne ni likizo ya familia kwa mzazi ambaye si mama aliyebeba ujauzito.
Tano ni Ruhusa kwa klabu kusajili mchezaji mpya nje ya dirisha la usajili ikiwa mchezaji wa kikosi yuko likizo ya uzazi au ulezi.
Sita ni haki ya kuomba kutoshiriki mazoezi au mechi kutokana na matatizo ya afya yanayohusiana na hedhi bila kupoteza mshahara.
Mwaka 2022, mshambuliaji wa zamani wa timu ya taifa wanawake ya England, Toni Duggan, alikua mchezaji wa kwanza wa 'Women's Super League' kupokea malipo ya uzazi akiwa mchezaji wa timu ya waawake ya Everton.
Aidha, mwezi uliopita, Shirikisho la wachezaji (PFA) ilianzisha ushirikiano na kliniki ya uzazi ili kuwasaidia wanachama wake kupata ushauri wa siri na wa kitaalamu kuhusu upangaji wa familia pamoja na punguzo la gharama za baadhi ya matibabu ya uzazi.