Pep anadaiwa alijaribu mara 100 kusepa City
Muktasari:
- Kwa mujibu wa mwenyekiti wa klabu hiyo, Khaldoon Al Mubarak, kocha huyo Mhispania aliwahi kufikiria kuondoka mara nyingi kabla ya kuamua msimu wa 2025/26 ungekuwa wa mwisho kwake.
BARCELONA, HISPANIA: KUONDOKA kwa Pep Guardiola Manchester City huenda kulionekana kama jambo la ghafla kwa baadhi ya mashabiki, lakini ukweli ni tofauti kabisa.
Kwa mujibu wa mwenyekiti wa klabu hiyo, Khaldoon Al Mubarak, kocha huyo Mhispania aliwahi kufikiria kuondoka mara nyingi kabla ya kuamua msimu wa 2025/26 ungekuwa wa mwisho kwake.
Ufichuzi huo umetoa mwanga kuhusu shinikizo kubwa la kihisia na kiakili linaloambatana na ukocha katika kiwango cha juu kabisa cha soka.
Guardiola alitumia miaka 10 akiiongoza Manchester City katika moja ya vipindi vya mafanikio makubwa zaidi katika historia ya mchezo huo, lakini nyuma ya mataji na sherehe kulikuwa na kocha ambaye mara kwa mara alikuwa akihoji uwezo wake wa kuendelea na kazi hiyo.
Akizungumzia kuondoka kwa Guardiola, Al Mubarak alisema kocha huyo aliwahi kutishia kuondoka “mara 100” katika kipindi chake cha uongozi na kila mara viongozi wa klabu walifanikiwa kumshawishi kubaki na kuendelea kujenga mradi uliogeuza Man City kuwa moja ya klabu kubwa zaidi duniani.
Baada ya miaka 10 ya ukocha kikosini hapo, Guardiola aliujulisha uongozi wa klabu kwamba safari yake ilikuwa imefika mwisho na uamuzi wake ulikuwa wa mwisho na mwenyekiti huyo alisema hawakuwa na jinsi kwa sababu huko nyuma walitumia nguvu nyingi kumzuia.
Kauli hiyo inaonyesha Guardiola kocha ambaye hakuwahi kuona mafanikio kuwa jambo rahisi au la kawaida na hivyo hakutaka kuendelea kung’ang’ania klabuni hapo.
Guardiola alipowasili Man City 2016, klabu hiyo tayari ilikuwa miongoni mwa timu bora England.
Hata hivyo, wakati anaondoka, alikuwa ameifikisha katika kiwango cha juu zaidi na chini ya uongozi wake City ilitwaa mataji mengi ya Ligi Kuu England, makombe ya ndani pamoja na Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Katika mahojiano ya hivi karibu alisema kuwa anatamani kuondoka kwenye majukumu ya ukocha kwa muda ili kupumzika baada ya kuzifundisha Barcelona, Bayern Munich na Manchester City akitumia karibu miongo miwili akiishi chini ya shinikizo kubwa na kila mechi, kila uamuzi na kila matokeo yalikuwa yakifuatiliwa kwa karibu.