Pep alia ugumu wa ratiba Man City
Muktasari:
- Man City imepangwa kumenyana na Real Madrid kwenye mchujo wa kusaka nafasi ya kutinga hatua ya 16 bora kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya ndani ya Februari, ambapo pia itakuwa na mechi za kibabe dhidi ya Arsenal, Newcastle na Liverpool.
MANCHESTER, ENGLAND: PEP Guardiola amedai hana sababu ya kulalamikia ratiba ngumu inayoikabili Manchester City kwa mwezi huu wa Februari kwa sababu siku zote England imekuwa na tatizo hilo miaka yote.
Man City imepangwa kumenyana na Real Madrid kwenye mchujo wa kusaka nafasi ya kutinga hatua ya 16 bora kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya ndani ya Februari, ambapo pia itakuwa na mechi za kibabe dhidi ya Arsenal, Newcastle na Liverpool.
“Ratiba ndiyo kama ilivyo,” alisema kocha huyo wa Man City na kuongeza. “Kwenye Ligi Kuu England kila timu ni lazima icheze na kila mtu, lakini kwa timu za hapa siku zote zimekuwa zikiwekewa mechi ngumu wakati huo zikiwa na michuano ya Ulaya iliyofikia kwenye hatua ngumu.
“Ni ngumu sana kucheza na Real Madrid au Bayern na tatizo katikati ya mechi kama hizo, unacheza na Newcastle. Siku zote imekuwa hivi kwenye ishu ya ratiba, kwa miaka mingi imekuwa hivyo.”
Guardiola alidai kwamba tatizo la ratiba kuwa ngumu kwenye Ligi Kuu England ni jambo la muda mrefu kabla hata hajatua Etihad, aliposema: “Nakumbuka, wakati nikiwa Barcelona, nilikuwa nafuatilia Ligi Kuu England kwa sababu ni ligi inayovutia duniani na makocha Sir Alex Ferguson, Jose Mourinho, Arsene Wenger wote walikuwa na malalamiko kama haya ya ratiba.”
Guardiola alisema ligi za nchi nyingine zimekuwa zikisaidia timu zao zinapokuwa na mechi za Ulaya kama vile Ureno na Ufaransa.