Penalti ya Bruno yaanzisha mjadala
Muktasari:
- Bruno Fernandes ni mmoja wa wapiga penalti mahiri kwenye Ligi Kuu England, ndiye mpigaji mkuu wa mikwaju hiyo kwenye kikosi cha Man United tangu alipowasili kujiunga na timu hiyo Januari 2020.
MANCHESTER, ENGLAND: MJADALA umeibuka huko Manchester United kuhusu chaguo la mchezaji wa kupiga penalti za timu hiyo zitakazopatikana kwenye mechi zao.
Bruno Fernandes ni mmoja wa wapiga penalti mahiri kwenye Ligi Kuu England, ndiye mpigaji mkuu wa mikwaju hiyo kwenye kikosi cha Man United tangu alipowasili kujiunga na timu hiyo Januari 2020.
Lakini, baada ya kukosa mkwaju wake dhidi ya Fulham, Jumapili iliyopita na kuigharimu Man United kukosa pointi tatu ni wakati wa kocha Ruben Amorim kufikiria upya na kuwapa nafasi mastaa wake wapya Bryan Mbeumo na Matheus Cunha, ambao pia ni mahiri kwenye kazi hiyo ya kupiga penalti.
Kiungo huyo Mreno, Fernandes sasa amefunga penalti 22 kati ya 27 alizopiga kwenye kikosi cha Man United katika Ligi Kuu England, ikiwa ni mafanikio ya asilimia 81.5. Si haba.
Anajumuika na kundi kubwa la mastaa hodari kwa mikwaju ya penalti. Supastaa wa Liverpool, Mohamed Salah ana wastani wa asilimia 85 wa kufanikiwa mikwaju yake, ambapo amefunga penalti 34 kati ya 40 alizopiga. Straika wa Manchester City, Erling Haaland ana wastani wa asilimia 89, akifunga penalti 17 kati ya 19 alizopiga kwenye Ligi Kuu England.
Kwenye historia ya Man United, Fernandes anapambana na magwiji Wayne Rooney (asilimia 71 baada ya kufunga 20 kati ya 28), wakati Ruud van Nistelrooy amefunga penalti 18 kati ya 22 alizopiga na hivyo kuwa na wastani wa asilimia 82 za kufanikiwa kuukwamisha mpira nyavuni.
Kwenye soka kwa ujumla, ukianzia kwenye vikosi vya Udinese na Sporting Lisbon, Fernandes amefunga penalti 35 kati ya 41 alizopiga na kuwa na wastani wa asilimia 85.4 kwenye kupachika mpira nyavuni kwa mikwaju hiyo.
Mbeumo, aliyesajiliwa kutokea Brentford kwa Pauni 71 milioni kwenye dirisha hili, amefunga penalti 10 kati ya 11 na kuwa na wastani wa asilimia 90.9 wa kupachika mipira nyavuni. Staa mwingine mpya, Cunha, aliyenaswa kwa Pauni 62.5 milioni, Mbrazili huyo alipokuwa Wolves alifunga penalti moja aliyopiga, wakati alipokuwa Hertha Berlin alifunga mbili kati ya tatu na hivyo kuwa na wastani wa asilimia 75 kwenye usahihi wa kupachika penalti zake nyavuni.