Panga la Pep kumgusa Gundogan

Muktasari:
- Mabingwa wa Uturuki, Galatasaray, ndio wanatajwa kutaka kumsajili Gundogan mwenye umri wa miaka 34, ambaye amebakiza mwaka mmoja katika mkataba wake wa sasa.
MANCHESTER, ENGLAND: KOCHA wa Manchester City, Pep Guardiola amefungua mlango kwa kiungo wao, Ilkay Gundogan kuondoka na kukiri Manchester City italazimika kuuza baadhi ya wachezaji majira haya ya kiangazi.
Mabingwa wa Uturuki, Galatasaray, ndio wanatajwa kutaka kumsajili Gundogan mwenye umri wa miaka 34, ambaye amebakiza mwaka mmoja katika mkataba wake wa sasa.
Kocha wa Man City, Guardiola, ambaye alimrudisha Gundogan msimu uliopita kwa awamu ya pili akitokea Barcelona, alisisitiza bado anataka kumtumia kiungo huyo wa kimataifa wa Ujerumani kwenye mipango yake kwa ajili ya Kombe la Dunia la Klabu.
Hata hivyo, Guardiola alikiri kikosi chake kwa sasa ni kikubwa mno na atalazimika kuachana na baadhi ya wachezaji ili kuwe na mazingira ya utulivu ndani ya vyumba vya kubadilishia nguo na kuepuka kuwa na majina makubwa mengi yasiyopata muda wa kucheza.
Alipoulizwa kuhusu hatma ya Gundogan, Guardiola alisema:"Sina cha kuwaambia kwa sasa, ila hizo ni habari njema. Lakini sijui chochote, sijaongea naye, lakini kwa sasa, tuna kikosi kipana sana, wachezaji wengi mno, hatuwezi kwenda na wachezaji 26 au 27 msimu huu kwa sababu wengine hawatapata nafasi ya kucheza. Hatua kwa hatua huenda baadhi ya wachezaji wakaondoka.”
"Lakini kwa sasa, Ilkay ni sehemu ya timu yangu. Ningependa kuendelea kuwa na wachezaji tulionao sasa msimu mzima. Ningependa hivyo. Sina malalamiko yoyote kuhusu tabia zao. Tatizo ni kuwa hawatakuwa na furaha msimu ukiendelea. Watakuwa na huzuni, watavunjika moyo. Sitaki hilo. Kwangu si tatizo, lakini sitaki kuwa na wachezaji sita au saba nyumbani tu, hawachezi. Nataka waondoke kwa ajili ya maisha yao."
"Bado tuna muda mrefu kabla dirisha la usajili kufungwa. Na ndio, tutaona hatua kwa hatua kitakachotokea.”
Man City pia inatarajiwa kuwaachilia nyota wawili wa England, Kyle Walker na Jack Grealish huku Rodri, ambaye amerudi uwanjani baada ya kupona jeraha kubwa la goti (cruciate ligament), bado akiendelea na mazoezi ya kurejea katika hali yake kamili.
Guardiola alisema jeraha la Rodri kwa kawaida linachukua kati ya miezi '10 hadi 12' kupona na anaamini huenda ikachukua miezi mingine mitatu kabla hajarejea katika ubora wake na kwa sasa, watakuwa wakimchezesha kwa tahadhari.