Pale Real Madrid kuna ‘utoto mwingi’
Muktasari:
- Inalezwa pia kauli hiyo ilichangia sana katika anguko lake kama kocha lakini aliwaambia ukweli hakuna mahali watafika ikiwa hawatobadilika.
MADRID, HISPANIA: WAKATI matokeo mabaya yakizidi kuiandama Real Madrid baada ya juzi kutolewa katika michuano ya Copa del Rey dhidi ya Albacete inayoshiriki Ligi Daraja la kwanza Hispania kwa mabao 3-2, inaripotiwa kocha wa zamani wa timu hiyo Xabi Alonso aliwahi kuwaambia wazi wachezaji wake kuwa wanatabia za watoto wa chekeche, hali inayosababisha timu kuwa kwenye hali yao ya sasa.
Inalezwa pia kauli hiyo ilichangia sana katika anguko lake kama kocha lakini aliwaambia ukweli hakuna mahali watafika ikiwa hawatobadilika.
Kocha huyo inadaiwa aliongea kwa hasira mbele ya mastaa wake mapema Novemba mwaka jana, wakati ambao alikuwa haelewani na kundi kubwa la wachezaji.
Alonso aliondolewa rasmi na Madrid, Jumatatu ya wiki hii ikiwa ni miezi saba tu baada ya kujiunga na klabu hiyo, huku kukiwa na taarifa nyingi, uhusiano wake na wachezaji ulishavurugika kwa asilimia kubwa licha ya Jude Bellingham na Kylian Mbappe kusema hakukuwa na shida yoyote.
Gazeti la Hispania, MARCA, linaripoti Alonso alikuwa tayari amashajikatia tamaa na alikuwa anasubiria simu ya kumfukuza kazi tangu wakati huo.
Alonso alikuwa anaona wachezaji wake wakiwa wachovu na hawapambani kama alivyohitaji jambo ambalo lilimfanya awaite watoto wa chekechea.
Zaidi ya hayo, MARCA indai kuwa taarifa kuhusu Alvaro Arbeloa kuja kumrithi Alonso lilianza kusikika katika kikosi muda mrefu kabla hajateuliwa rasmi.
Arbeloa alikuwa kocha wa timu ya pili ya Madrid na alikuwa akihudhuria mara kwa mara mazoezi ya timu ya kwanza.
Chini ya Alonso, mastaa wa Madrid walidai vipindi vya darasani vya mafunzo ya mbinu vilikuwa ni virefu na vingi kupita kiasi, wakilalamikia kumezeshwa mambo mengi, hadi wengine wakawa wanakosa utulivu kutokana na maelekezo hayo mengi kupita kiasi.
Alonso alikuwa anapitia wakati mgumu kuwashawishi mastaa kama Kylian Mbappe na Vinicius Junior kuamini katika falsafa ya pamoja iliyofanya kazi vizuri Bayer Leverkusen.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 44 alifukuzwa kazi chini ya saa 24 baada ya kupoteza fainali ya Super Cup ya Hispania kwa mabao 3-2 dhidi ya Barcelona huko Jeddah, Saudi Arabia.
Alikuwa chini ya presha kubwa kutokana na tetesi za mgogoro na baadhi ya wachezaji pamoja na kutofautiana kimtazamo na uongozi wa klabu kuhusu mbinu zake.
Hata hivyo, rekodi yake haikuwa mbaya sana. Madrid bado wanapigania ubingwa wa LaLiga na wanashika nafasi ya saba katika ligi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Moja ya matukio yaliyoonyesha udhaifu wake wa mamlaka lilitokea baada ya fainali ya Super Cup na Alonso alitaka wachezaji wake waifanyie Barcelona guard of honour, lakini Mbappe alikataa na hatimaye kocha alilazimika kurudi nyuma.
Baadaye, Mbappe amesema ilikuwa 'furaha' kufanya kazi na Alonso.
Kwa upande mwingine, Bellingham amekanusha vikali madai kuwa aligombana na kocha huyo.
“Hadi sasa nimekuwa nikiyapuuzia maneno mengi sana, nikiamini ukweli utajitokeza kwa wakati wake,” aliandika Bellingham kupitia mitandao yake ya kijamii.