Paddy Kenny amwita Rooney ulingoni
Muktasari:
- Kipa huyo ambaye aliwahi kupita pia Leeds na akaichezea timu ya taifa la Ireland, anadai Rooney amekuwa akimkashifu na kusema aliachia ili afungwe makusudi bao na Sergio Aguero mwaka 2012 na kusababisha Man United ipoteze taji.
MANCHESTER, ENGLAND: LEJENDI wa Manchester United, Wayne Rooney amealikwa katika pambano la ngumi na kipa wa zamani wa Sheffield United, Paddy Kenny.
Kipa huyo ambaye aliwahi kupita pia Leeds na akaichezea timu ya taifa la Ireland, anadai Rooney amekuwa akimkashifu na kusema aliachia ili afungwe makusudi bao na Sergio Aguero mwaka 2012 na kusababisha Man United ipoteze taji.
Kenny atakuwa na mpambano dhidi ya mchezaji mwingine wa zamani wa Ligi Kuu England, Curtis Davies, ambalo litakuwa ni la hisani lakini yeye anamtamani zaidi Rooney.
Akizungumza na Boxing Social, Kenny alisema: "Ananikashifu sana kuhusu bao la Aguero, kwa hiyo nadhani mimi na yeye tunahitaji kutatua hili ndani ya ulingo. Baada ya miaka 13, bado anasema niliruhusu makusudi! Lakini ukweli haikuwa hivyo."
Awali Rooney mwenye umri wa miaka 39, aliwahi kupatiwa nafasi ya kuingia kwenye ulingo na kampuni ya Misfits Boxing mwaka jana kabla ya kuajiriwa na Plymouth Argyle mwaka jana, lakini alikataa na kusisitiza kwa sasa bado anatamani zaidi kufundisha.
"Waliwasiliana na mimi na kuulizia ikiwa naweza kupanda ulingoni, lakini kwa sasa nataka kufundisha zaidi siyo kupigana," alisema Rooney.
Tangu aachane na Plymouth, Rooney amekuwa akifanya kazi ya uchambuzi katika kipindi cha Match of the Day na haijajulikana ikiwa kwa sasa atakuwa tayari kuingia ulingoni au bado ataendelea kusubiria timu ya kuifundisha ambalo ndio jambo analotamani zaidi.
Kenny amekuwa akipigana mapambano mbalimbali ya hisani kwa ajili ya kukusanya pesa zinazotumika kusaidia jamii na pambano lake dhidi ya Rooney ikiwa litatokea linaweza kuwa na mazingira hayo.