Rooney: Amorim hana visingizio tena
Muktasari:
- Licha ya kutumia Pauni 200 milioni katika dirisha hili la majira ya kiangazi, Man United imekusanya pointi moja tu katika mechi zake mbili za mwanzo za Ligi Kuu England msimu huu.
MANCHESTER, ENGLAND: LEJENDI wa Manchester United, Wayne Rooney amesema Ruben Amorim hana tena visingizio na lazima ahakikishe timu inaanza kupata matokeo haraka.
Licha ya kutumia Pauni 200 milioni katika dirisha hili la majira ya kiangazi, Man United imekusanya pointi moja tu katika mechi zake mbili za mwanzo za Ligi Kuu England msimu huu.
Rooney ambaye ni mfungaji bora wa muda wote wa klabu hiyo anakiri kuwa anahofu kwa sababu anaona baadhi ya dalili zilezile za msimu uliopita.
Amorim amepata pointi 28 tu katika michezo yake 29 ya ligi tangu achukue mikoba Novemba mwaka jana, huku mafanikio pekee aliyokuwa nayo ni kufika fainali ya Europa League msimu uliopita.
Baada ya sare dhidi ya Fulham waliyopata wiki iliyopita, Rooney alisema: "Hakuna visingizio tena kwa kocha msimu huu. Amepewa kila kitu, sasa lazima aanze kupata matokeo, tena kwa haraka.
"Ukianza kuingia Oktoba au Novemba na matokeo haya haya kwa kiasi kikubwa, hapo ndipo presha itakapoongezeka. Walitakiwa kuanza msimu kwa kishindo, lakini pointi moja kati ya sita inaleta wasiwasi."
Alipoulizwa kama Amorim ndiye mtu sahihi wa kuirudisha timu katika enzi zake, Rooney aliongeza: "Ni vigumu kukaa hapa na kusema ‘Ndiyo kwa asilimia 100’. Sidhani kama kuna mtu yeyote anaweza kusema hivyo. Hata Ruben mwenyewe pengine hawezi kusema hivyo kutokana na tulichokiona tangu ajiunge na klabu. Nafikiri usajili wa majira ya kiangazi ulikuwa mzuri, ingawa bado ningependa kuona wachezaji wawili au watatu zaidi wakisajiliwa. Lakini ni vigumu kusema huyu ndiye atakuwa kocha wetu kwa miaka mitano ijayo kutokana na kile tulichokiona hadi sasa.
"Huenda ninaharakisha mambo kuyasema haya sasa lakini nimeanza kupata wasiwasi kwa sababu ninaona ishara za mambo yale tuliyoyaona msimu uliopita ingawa bado tupo kwenye mechi mbili tu za mwanzo. Hilo ndilo linatia hofu."