Owen Hargreaves: Chelsea inatakiwa kumsajili Marquinhos
Muktasari:
- Licha ya kutumia karibu pauni 300 milioni katika usajili wa wachezaji majira ya joto, Chelsea imeanza msimu mpya kwa kusuasua ikiwa nafasi ya nane baada ya kucheza mechi sita, ikishinda mara mbili na kupoteza mara mbili.
KIUNGO wa zamani wa Manchester United, Owen Hargreaves, anaamini kuwa Chelsea inahitaji kuongeza mchezaji mmoja katika nafasi ya mlinda mlango na mwingine beki wa kati, iwapo wanataka kutwaa mataji ya Ligi Kuu England na Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu 2025-2026.
Chelsea ilimaliza msimu wa 2024-2025 kwa mafanikio mazuri chini ya kocha Enzo Maresca, ikitwaa UEFA Conference League na Kombe la Dunia la Klabu la FIFA. Aidha, ilimaliza nafasi ya nne kwenye ligi, ikiwa pointi 15 nyuma ya mabingwa Liverpool, ingawa awali ilikuwa inachuana kwa karibu na miamba hiyo ya Anfield katika mbio za ubingwa, lakini iliishiwa nguvu nusu ya pili ya msimu.
Licha ya kutumia karibu pauni 300 milioni katika usajili wa wachezaji majira ya joto, Chelsea imeanza msimu mpya kwa kusuasua ikiwa nafasi ya nane baada ya kucheza mechi sita, ikishinda mara mbili na kupoteza mara mbili.
Hargreaves, akizungumza na TNT Sports (kama alivyonukuliwa na The Metro), amesema Chelsea inahitaji kuimarisha safu ya ulinzi kwa kuleta mchezaji mwenye uzoefu kama beki wa kati. Amemtaja beki wa Paris Saint-Germain (PSG), Marquinhos, kama chaguo sahihi
"Kama Chelsea wanataka kutwaa EPL na UEFA, wanahitaji kipa wa kiwango cha dunia na beki wa kati mwenye uzoefu. Kwa beki wa kati, mchezaji kama Marquinhos anaweza kuwasaidia hawa vijana," amesema.
Marquinhos bado ana mkataba na PSG hadi mwaka 2028, jambo linalofanya usajili wake kuwa mgumu, lakini si jambo lisilowezekana ikiwa Chelsea itaamua kuwekeza kikamilifu.