Cole Palmer ambwaga Ronaldo, amtaja Ravel Morrison
Muktasari:
- Badala yake, Palmer amemchagua kiungo wa zamani wa Man Utd U18, West Ham, Lazio na timu kadhaa ikiwemo ADO Den Haag, Ravel Morrison, ambaye amewahi kutajwa kuwa na kipaji kikubwa lakini hakutimiza matarajio hayo.
NYOTA wa Chelsea, Cole Palmer, ametaja kikosi chake cha wachezaji watano bila kumjumuisha Cristiano Ronaldo jambo lililowashangaza wengi.
Badala yake, Palmer amemchagua kiungo wa zamani wa Man Utd U18, West Ham, Lazio na timu kadhaa ikiwemo ADO Den Haag, Ravel Morrison, ambaye amewahi kutajwa kuwa na kipaji kikubwa lakini hakutimiza matarajio hayo.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa England mwenye umri wa miaka 23, ametaja jina lake mwenyewe pamoja na Thibaut Courtois, Lionel Messi, Neymar na Morrison kwenye kikosi cha ndoto zake.
Kumchagua Morrison ambaye alionekana kama mchezaji aliyeanguka licha ya kuanza na matumaini makubwa, kumezua mshangao mkubwa kwa mashabiki waliofuatili orodha ya Palmer.
Ravel Morrison alitokea kwenye akademi ya Manchester United lakini aliichezea timu ya wakubwa mechi tatu pekee. Katika Premier League, alicheza jumla ya mechi 18 tu, akiwa na West Ham na Sheffield United.
Baada ya hapo, aliondoka England na kutimkia Italia, Sweden, Marekani, Mexico na Falme za Kiarabu.
Mara ya mwisho aliichezea Precision FC inayoshiriki Ligi Kuu Falme za Kiarabu (UAE Second Division League), na kwa sasa hana klabu.
Alikuwa na matumaini makubwa akiwa kinda, alicheze timu za taifa za vijana za England, lakini hakuwahi kucheza kwa timu ya wakubwa. Baadaye aliamua kuitumikia timu ya taifa ya wakubwa ya Jamaica, ambako alicheza mechi 21. Kwa sasa ana umri wa miaka 32 akiwa hana timu.