Osimhen adhamiria kuivusha Nigeria Kombe la Dunia 2026
Muktasari:
- Osimhen alitangaza msimamo huo, baada ya Galatasaray kupoteza kwa bao 1–0 dhidi ya Kocaelispor katika Ligi Kuu ya Uturuki jana Jumapili, Novemba 09, 2025.
Mshambuliaji wa Galatasaray, Victor Osimhen, amesema hana budi kusahau matokeo ya klabu hiyo na kujipanga kwa ajili ya majukumu ya timu ya taifa ambapo Nigeria inajiandaa kuikabiliana Gabon katika mechi ya mchujo wa Kombe la Dunia, Novemba 13, 2025.
Osimhen alitangaza msimamo huo, baada ya Galatasaray kupoteza kwa bao 1–0 dhidi ya Kocaelispor katika Ligi Kuu ya Uturuki jana Jumapili, Novemba 09, 2025.
Mshambuliaji huyo alishindwa kuisaidia Galatasaray kwenye mechi hiyo ugenini licha ya kuonyesha juhudi kubwa, huku bao pekee la Kocaelispor likifungwa na Dan Agyei katika Uwanja wa Kocaeli na kuwapa wenyeji ushindi.
Osimhen amesema kupoteza mechi ni jambo la kawaida japo imewauma sana, kwa sababu hawakutarajia hali hiyo kama ingetokea, lakini kwa sasa anajipanga kwa ajili ya jukumu la kuiwezesha Nigeria ifuzu Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Gabon.
“Mechi ya jana imeshapita, imetuuma kupoteza lakini ndio hivyo mambo yalivyo katika soka, sina budi kujipanga kwa ajili ya mechi muhimu ya taifa langu la Nigeria,” amesema Osimhen.
“Inanibidi kusafiri na kurudi nyumbani haraka, tayari kwa maandalizi ya mwisho ya kikosi cha Nigeria. Ninaamini haitakuwa mechi rahisi kwetu na kwa Gabon pia, lakini kusudi la Super Eagles ni kushinda mchezo huo ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kufusu Kombe la Dunia 2026.”
Mechi kati ya Nigeria na Gabon inatarajiwa kuanza saa 1:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki, kwenye Uwanja wa Hide Moulay Hassan nchini Morocco.
Timu ya taifa ya Nigeria maarufu Super Eagles ilimaliza hatua ya makundi ya kufuzu Kombe la Dunia la FIFA 2026 ikiwa katika nafasi ya pili kwenye Kundi C, ambapo ilikabiliana na Afrika Kusini, Rwanda, Lesotho, Benin, na Zimbabwe.
Licha ya kuanza kwa kusuasua kwa kupata sare na kupoteza baadhi ya mechi za awali, Nigeria ilijipanga na kurejea kwenye ushindani kupitia matokeo bora katika michezo ya mwisho, jambo lililowawezesha kumaliza nyuma ya kinara wa kundi Afrika Kusini.
Kwa upande wa timu ya taifa ya Gabon ilimaliza hatua ya makundi ya kufuzu Kombe la Dunia la FIFA 2026 ikiwa katika nafasi ya pili kwenye Kundi F la ukanda wa Afrika, ambalo lilijumuisha timu za Ivory Coast, Gabon, Kenya, Gambia, Burundi na Seychelles.
Gabon ilianza vizuri kwa kupata ushindi muhimu katika michezo ya awali, ikionyesha nidhamu nzuri ya kiufundi na safu imara ya ulinzi. Hata hivyo, ilikosa alama muhimu katika mechi za mwisho dhidi ya Ivory Coast na Kenya, hali iliyoifanya ishindwe kuongoza kundi hilo.