NYUMA YA PAZIA: Pep katika mbio zake za Duma, mateso kwa Arteta

Muktasari:

  • Unadhani ni mnyama mwenye kasi peke yake? Hapana. Wengine wapo lakini yeye ana kasi zaidi. Ananikumbusha Pep Guardiola na ligi yake ya England. Sio kwamba peke yake ni bora, hapana. Wapo wengine ila yeye ni bora zaidi. Anakimbia zaidi kuliko wenzake. Kamuulize mtu anayeitwa Jurgen Klopp atakwambia.

Anakimbia kilomita 133 kwa saa. Wapo ndege kadhaa wameipita kasi yake, lakini huku ardhini anabaki mnyama mwenye kasi zaidi duniani. Waswahili wanamuita duma, lakini Wazungu wanamuita cheetah.

Unadhani ni mnyama mwenye kasi peke yake? Hapana. Wengine wapo lakini yeye ana kasi zaidi. Ananikumbusha Pep Guardiola na ligi yake ya England. Sio kwamba peke yake ni bora, hapana. Wapo wengine ila yeye ni bora zaidi. Anakimbia zaidi kuliko wenzake. Kamuulize mtu anayeitwa Jurgen Klopp atakwambia.

Inawezekana kazi hii kwa sasa amemuachia Mikel Arteta. Apambane naye. Jumanne usiku Mikel Arteta alikuwa katika ubora wake akimchapa Chelsea mabao 5-0 pale Emirates. Akamuacha Pep kwa pointi nne, huku Pep akiwa na mechi mbili mkononi. Pep akaonekana ana kazi ngumu ugenini kwa Brighton. Kilichomtokea Brighton wote tunakijua. Na sasa Pep anahema katika sikio la Arteta. Yuko nyuma kwa pointi moja huku akiwa na mechi mkononi. Na sasa Arteta ana kasi ya kumfukuza duma. Hapaswi kupoteza mechi huku akiombea City aangushe pointi mbili kwa kutoa walau sare moja tu. Hapa ndipo utampenda Pep. Hapa ndio utajua mbio zake. Sio kwamba wanaomfukuza hawana mbio, hapana. Ila yeye ana kasi zaidi.

Hapa unarudi kwa Klopp. Namna alivyowahi kuitengeneza moja kati ya Liverpool bora katika historia. Sadio Mane, Roberto Firmino na Mo Salah wakiwa mbele. Wamepambana hasa na Pep, lakini hadi leo wakati Klopp akitangaza kuondoka England mwishoni mwa msimu huu ameishia kutwaa taji moja la EPL mbele ya Pep. Bila ya Pep naamini Klopp angekuwa na mataji kama manne hivi ya Ligi Kuu England. Pointi zake zilitosha mara zote tatizo duma alikuwa mbele yake. Pointi ambazo Sir Alex Ferguson na Arsene Wenger walikuwa wanachukulia ubingwa Pep amezifanya ziwe za mshindi wa pili. Msimu wa 2021/22 Pep alitwaa Ligi Kuu England akiwa na pointi 93, huku Liverpool ikiwa na pointi 92. Papo hapo kumbuka kwamba kikosi cha Arsenal kinachoimbwa, kile ambacho kilicheza msimu mzima bila ya kupoteza mechi kilimaliza ligi kikiwa na pointi 90 tu. Hapa ndipo utajua kitu ambacho Pep amefanya kwa wenzake katika ligi hii. Vipi kwa Sir Alex? Alikuwa anaonekana mbabe katika wakati wake. Mwaka 1999 aliishangaza dunia kwa kuchukua mataji matatu. Lakini labda nikwambie tu kwamba alichukua taji la Ligi Kuu England akiwa na pointi 79 tu. Arsenal ambao walikuwa wa pili walikuwa na pointi 78. Leo pointi 79 haziwezi kukupa ubingwa wa England kama Pep yupo katika ardhi ya Waingereza.

Hii ndio kazi ambayo inamkabili Arteta kwa sasa. Msimu uliopita angeweza kuchukua ubingwa kama Pep asingekuwepo katika soka la England. Hata msimu huu kama angekuwa anashindana na Klopp pekee ungeweza kusema kwamba alikuwa anatarajiwa kuwapa Arsenal taji la kwanza tangu mwaka 2004. Hata hivyo juu yao amesimama Pep.

Na sasa Arsenal imebakiza mechi nne wakati City ina mechi tano. Arteta anakabiliwa na moja kati ya kazi ngumu maishani kuliko hata alivyokuwa mchezaji. Hii ni kazi ngumu zaidi. Kazi ya kumfukuza duma ukampata ukampita mwendo. Ni kazi ngumu lakini mwanadamu lazima aifanye.

Na swali kubwa zaidi linalobaki kwa mashabiki ni hadi lini hali hii itaendelea? Pep anaonekana kuwa bado yupo yupo pale City. Mkataba wake unamalizika mwaka ni 2025. Hata hivyo, haonekani kama ataondoka ghafla kama ambavyo Klopp amefanya. Tetesi hizo hazipo kwa sasa. Tetesi zilizopo ni kwamba anaweza kuendelea kuwepo.

Lakini hauhitaji sana kujua kama bado yupoyupo. Kuna wachezaji ambao wanaelekea City unajua kabisa kwamba mwelekeo wa Pep ni kuendelea kubaki City. Mchezaji kama Savio ambaye anaelekea City kutoka Girona ni mchezaji wa aina ya Pep. Na kule Girona mmoja kati ya mabosi ni Pere Guardiola, kaka wa Pep.

Haiwezekani Pep akatengeneza njia hii kwa kocha ajaye wa City. Lazima ni mwendelezo wa kuja kuchukua nafasi za kina Bernardo Silva ambao muda wowote wanaweza kuondoka zao pale Etihad. Inaonekana kuna mchakato wa kutengeneza Manchester City mpya baada ya hii ambayo kila siku inasababisha pointi za kina Klopp na Arteta kuwa hazitoshi kila msimu.

Kuna Lucas Pacqueta wa West Ham United naye anatajwa kwamba amefikia makubaliano na Pep kwenda Manchester City. Huyu anatuachia swali zito kwa sababu ujio wake unaonekana ni kwa sababu ya uwezekano wa kuondoka kwa Kevin De Bruyne. City wataweza kuliziba pengo la De Bruyne akiondoka? Ni swali. Pep huwa anatengeneza timu yenye ubora mwingi lakini kuna wachezaji wachache ambao wanasimama na kuhesabiwa zaidi.

Pale Barcelona alitengeneza kikosi bora, lakini Lionel Messi akasimama na kuhesabiwa zaidi.

Ni kama sasa hivi pale City ametengeneza timu ya ajabu, lakini De Bruyne amesimama  kuhesabiwa. Kuna mchezaji anaweza kuwa De Bruyne mpya kama mwenyewe akiondoka zake kwenda kuchukua noti za Waarabu mwishoni mwa msimu? Ni swali la kujiuliza.

Kabla hatujafika huko kwa sasa ni wakati wa kujiuliza namna gani ambavyo Arteta anaweza kukabiliana na Pep kuanzia sasa hadi mwishoni mwa msimu. Tunataka kuona ziara zake za White Hart Lane nyumbani kwa wapinzani wa jadi Tottenham Hotspurs na kisha Old Trafford kama zinaweza kuzaa matunda katika kiu ya kumkimbiza Pep.

Spurs hawawezi kukubali Arteta apite pale na kuelekea katika mbio za ubingwa. Ni Simba na Yanga wa London. Lakini Manchester United naye atakuwa na roho mbili.

Roho ya kwanza ni kutaka Arsenal apite aende zake kwa sababu City ni majirani wenye kelele. Ni wapinzani wao wa jadi ambao kadri wanavyofanikiwa ndivyo wanavyowapigia kelele.

Lakini hapo nyuma Arsenal walishawahi kuwa wapinzani wao wakubwa. Kuona kwamba kwa sasa Arsenal wapo mbele yao na wao wapo nyuma ni kitu ambacho kinawaumiza. Hawapendi kuona sana.