Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

NYUMA YA PAZIA: Muda wa Wayne Rooney ‘Wazza’ kupumua katika sofa

Muktasari:

  • Kiwango kilekile cha kufunga mabao 30 katika mechi 30 kwenye ubora wake ndicho kiwango kilekile cha udhaifu akiwa katika kazi ya ukocha. Ndicho kiwango cha udhaifu ambacho kimeona Rooney akitimuliwa na timu nne katika miaka minne. Kweli Mungu hakupi kila kitu.

UNGEKUWA na wasiwasi kuweka pesa zako katika kampuni yoyote ya kamari ukiwa katika upande unaosema Wayne Rooney hawezi kufunga mabao 30 katika mechi 30. Katika ubora wake ungesita. Usingetia pesa yako. Moyo ungekuenda mbio kila anapojitokeza katika mlango wa kuingilia Old Trafford au uwanja wowote wa soka.

Kiwango kilekile cha kufunga mabao 30 katika mechi 30 kwenye ubora wake ndicho kiwango kilekile cha udhaifu akiwa katika kazi ya ukocha. Ndicho kiwango cha udhaifu ambacho kimeona Rooney akitimuliwa na timu nne katika miaka minne. Kweli Mungu hakupi kila kitu.

Uwanjani angeweza kuhaha. Angeweza kufunga mabao ya aina zote, kukaba, kupiga pasi za mwisho kiasi cha kuwanga’risha kina Cristiano Ronaldo, Carlos Tevez, Dimitar Berbatov, Robin Van Persie na wengineo lukuki. Rooney ni mchezaji wangu bora wa muda wote katika Ligi Kuu England na mimi ni shabiki wa Arsenal.

Katika benchi Rooney hatujui alikuwa anaelekeza nini wachezaji wake. Hatujui kwa kweli. Mbinu za kocha ni siri. Uchezaji wa mchezaji sio siri na ndio maana wote tunaelewa Rooney alikuwa mchezaji wa aina gani. Katika uwanja wa mazoezi hatujui alikuwa anawaelekeza nini wachezaji wake. Hata hivyo, matokeo ya alichokifanya katika uwanja wa mazoezi hayakuwa siri.

Juzi Rooney ametimuliwa na klabu yake ya Plymouth Argyle ya Daraja la Kwanza. Katika mechi 24 ameshinda mechi nne tu. Amewaacha wakiwa chini ya msimamo wakitaka kwenda Ligi Daraja la Pili ya England. Hatujui kuhusu kocha atakayekuja katika timu hiyo, lakini ni wazi kwamba Plymouth wangemchekea Rooney angewashusha.

Januari, mwaka jana, alifukuzwa na Birmingham City. Katika mechi 15 alikuwa ameshinda mechi mbili tu. Wakamwambia inatosha. Kabla ya hapo alikuwa akivurunda na Derby County ambayo ilikuwa imemchukua kutoka Marekani alikokuwa anafundisha DC United ya pale Washington. Huyu ndiye Rooney aliyewahi kuwa mmoja kati ya wachezaji hodari katika soka.

Kwanini anapata hizi kazi? Nadhani si ajabu kwa sababu yeye ni Wayne Rooney ‘Wazza’. Sioni sababu nyingine za yeye kupewa timu. Alikotoka haonyeshi rekodi nzuri, lakini nadhani anapata timu kwa sababu yeye ni Wayne Rooney. Ana mvuto wake. Anaongeza mvuto katika timu. Mmoja kati ya wachezaji bora wa muda wote Manchester United. Mfungaji bora wa muda wote Manchester United.  Hata hivyo, nadhani hii kazi ya kufundisha soka imemshinda.

Anaingia katika mkumbo wa wachezaji wengi mahiri wa zamani ambao wameshindwa kufanya vizuri katika kazi hii mpya ya kufundisha soka. Hizi ni kazi mbili tofauti. Kucheza soka na kufundisha soka ni kazi mbili tofauti. Kuna mastaa wa kila pembe ya dunia wameshindwa kazi hii ya pili kama tunavyoshuhudia ikimshinda Rooney.

Tusiende mbali. Tubaki palepale England. Kina Steven Gerrard, Frank Lampard, Roy Keane na wengineo hawakuweza kazi hii mpya licha ya umahiri wao mkubwa katika soka. Kazi hii tofauti ilikuja kuwa maji marefu kwao. Hakuna ambaye alikaribia kuja kuwa Pep Guardiola mpya katika ukocha.

Waingereza walikuwa wapiga debe wa mastaa wao katika kazi ya ukocha. Walitamani siku moja Gerrard afundishe Liverpool, Lampard afundishe Chelsea, Rooney afundishe Manchester United. Ni katika kile ambacho waliamini kingekamilisha hadithi tamu baina ya mchezaji na timu yake. Kama vile Pep Guardiola na Barcelona. Kama vile Zinedine Zidane na Real Madrid. Haikuwezekana.

Sijui kwanini kazi ya ukocha inawashinda hawa mastaa wengine hasa wa Kiingereza. Kuandaa timu? Kupanga utawala wa timu? Kusoma mbinu za wapinzani? Haya yote wakati unacheza unaletewa mezani na Sir Alex Ferguson ambaye anakuwa ameyafanyia kazi na wasaidizi wake. Sasa umefika muda wa wewe kuyapanga hayo ili wachezaji wako wayafanyie kazi. Hii inakuwa kazi mpya na tofauti.

Kuna watu hawakutaka kuigusa kazi hii. Hayati Pele hakuwahi kuigusa. Pale katika makochi Rio Ferdinand na Jamie Carragher hawakujaribu hata kuigusa. Nadhani machale yaliwacheza kwamba ilikuwa kazi tofauti na ile ya kucheza au kukaa katika makochi.

Na sasa ni muda wa Rooney kurudi katika makochi akaungane na kina Gary Neville, Rio Ferdinand, Jamie Carragher, Roy Keane, Thierry Henry kufanya kazi ya uchambuzi studio. Hii ni kazi rahisi. Unatazama makosa au ubora wa kile kilichoandaliwa na kocha. Unatazama upungufu wa wachezaji au waamuzi huku ukiwa umekaa katika kochi.

Kazi ya ukocha ni kutabiri kinachoweza kutokea. Kazi ya uchambuzi ni kusubiri kwanza makosa yatokee kisha unayaelezea kwa urahisi tu. Neville akiwa kocha pale Valencia alifukuzwa ndani ya miezi sita tu. Akiwa katika makochi pale Skysport anakuwa mmoja kati ya wachambuzi bora kuwahi kutokea katika soka.

Haishangazi kuona kuna bifu kubwa kati ya makocha na wachambuzi. Jose Mourinho ni mmoja kati ya makocha ambao wanawapuuza wachambuzi kwa namna ambavyo wenyewe wamefeli au wameshindwa kuingia katika kazi ngumu ya ukocha na badala yake wanakaa katika makochi kuchambua kazi ngumu za makocha.

Wayne Rooney naye baada ya kufukuzwa tu nasikia kuna vituo mbalimbali vya televisheni vinamuwania akakae katika sofa na kwenda kuifanya kazi nyingine mpya ambayo anaweza kuifanya kwa ufasaha kama ile kazi yake ya kwanza maishani. Hii ya hapa katikati ni wazi kwamba imemshinda kama ilivyowashinda kina Neville. Na afadhali akampumzike katika makochi kwa sababu kazi hii inaweza kumpumzisha zaidi hata katika masuala ya kinidhamu. Kazi ya ukocha na uchezaji ilimlazimisha awe na wakati mgumu kuwa na nidhamu. Rooney ni mtu wa pombe na wakati mwingine amekuwa akifumwa na mabinti. Siku moja kabla hajafukuzwa na Plymouth alionekana akimuingiza mwanamke katika ‘apartment’ anayoishi.

Labda katika kazi ya sofa itampa muda pia wa kupiga kinywaji na washkaji zake bila ya kuwahi kuamka kwenda mazoezini kama ilivyokuwa inamlazimu akiwa mchezaji na baadaye kocha. Labda pia mkewe, Coleen atapata wakati mzuri wa kuwa karibu na mumewe tofauti na ilivyotokea katika kazi ya ukocha.

Tusisahau pia kwa Rooney kufeli kunatukumbusha namna ambavyo Sir Alex Ferguson ameshindwa kutoa makocha wa maana miongoni mwa wachezaji aliowahi kuwafundisha soka. Karibu wote wamefeli au wamekuwa makocha wa kawaida tu. Kina Keane, Neville, Steve Bruce, Paul Ince na wengineo wengi. Afadhali David Beckham aliamua kwenda kumiliki timu Marekani.